Utitiri wa kodi wawakera wafanyabiashara

28Feb 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Utitiri wa kodi wawakera wafanyabiashara

UTITIRI wa kodi kwa wafanyabiashara na wawekezaji mkoani Shinyanga umedaiwa kuwa kero na kusababisha mapato kidogo na baadhi wakidai kuzifunga biashara zao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda, na Kilimo (TCCIA), mkoani Shinyanga, Meshack Kulwa, alisema hayo wakati akisoma taarifa kwenye mkutano wa mashauriano kati ya serikali, wafanyabiashara na wawekezaji mkoani humo.

Alisema kero kubwa wanayokabiliana nayo wafanyabiashara na wawekezaji mkoani humo ni utitiri wa kodi ambao unasababisha baadhi yao kushindwa kuzimudu kulipa, huku wengine wakifunga na kufungiwa baadhi ya biashara zao kwa sababu ya kushindwa kulipa kodi hizo.

“Kero kubwa dhidi ya wafanyabiashara na wawekezaji ni kuwapo kwa utitiri wa kodi, hivyo tunachokiomba kwa serikali ituondolee zile kodi ambazo ni kero, ili nasisi tuendelee kufanya biashara tukue kiuchumi na kulipa kodi,” alisema Kulwa.

“Pia tunaomba pale kunapotokea mgogoro wa ulipaji kodi kati ya mfanyabiashara na serikali, itafutwe suluhu na hata kupitia kwenye chama chetu cha TCCIA, na siyo kwenda tu kufunga biashara au kiwanda, na kisha kutuchafua kwenye vyombo vya habari,” aliongeza.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema, serikali itaendelea kuzifuta kodi, tozo na ushuru ambazo ni kero kwa wafanyabiashara, ili zibaki zinazoweza kulipika, ikiwa hakuna ukusanyaji wa mapato serikalini bila kuwapo na wafanyabiashara wala wawekezaji.

Alisema kwa kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais John Magufuli, wamefuta kodi, tozo na ushuru 168 ambazo zilikuwa kero kwa wafanyabiashara, lakini cha ajabu mapato yamezidi kuongezeka, tofauti na hapo awali kwa sababu walipakodi walikuwa wachache kwa kukwepa kulipa kodi kutokana na utitiri huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia uwekezaji, Anjellah Kairuki, alisema serikali itazishughulikia kero zote zilizotolewa na wafanyabiashara hao likiwamo suala la utitiri wa kodi na tozo mbalimbali, huku akiwataka viongozi wa serikali kufuata taratibu za ufungaji wa biashara, na wafanyabiashara nao walipe kodi kwa hiari.

Pia alitoa wito kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza mkoani Shinyanga, ambapo kuna fursa nyingi ya viwanda vya nguo, na ngozi, huku akipongeza utengwaji wa maeneo mengi kwa ajili ya uwekezaji, na kubainisha ndiyo sera hasa ya rais kuhakikisha wawekezaji hawapati shida ya maeneo na yasiwe na mgogoro.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, awali wakati akifungua mkutano huo, alisema serikali mkoani humo imefungua milango ya wawekezaji wa malighafi ya pamba na ngozi na wameshatenga maeneo ya uwekezaji hekta 20,289.25 na yote wameshalipa fidia na hayana mgogoro.

Habari Kubwa