Utoaji leseni migodi mikubwa wakamilika

28Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Utoaji leseni migodi mikubwa wakamilika

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini inakamilisha taratibu za utoaji wa leseni kwa migodi mikubwa ambazo hazijawahi kutolewa nchini, huku migodi hiyo ikitarajiwa kuanzishwa hivi karibuni.

Hayo yalibainishwa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, alipokutana na viongozi wa jumuiya ya watendaji wakuu wa taasisi binafsi ofisini kwake, jijini Dodoma.

Viongozi hao walikutana na Prof. Msanjila kwa lengo la kujitambulisha, kuelewa shughuli za serikali upande wa sekta ya madini, kupata uelewa kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Madini na namna pande hizo mbili zinavyoweza kushirikiana katika kuendeleza sekta husika.

Prof. Msanjila aliwakaribisha viongozi hao kwenye sekta ya madini, huku akiwataka kuzishawishi kampuni mbalimbali kuwekeza nchini hususani katika shughuli za uongezaji thamani madini na kueleza kuwa suala hilo ni miongoni mwa maeneo ambayo serikali inayapa kipaumbele ikiwamo ujenzi wa vinu vya kusafisha na kuyeyusha madini.

Kuhusu Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, Prof. Msanjila alisema hakuna tatizo lolote katika utekelezaji wa sheria na kueleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Madini inapokea wawekezaji wengi wenye utayari na nia ya kuwekeza nchini, huku utekelezaji wa sheria hiyo ukiwa si kikwazo.

“Hakuna mahali ambapo serikali inatengeneza sheria kwa ajili ya kumkandamiza mfanyabiashara,” alisema na kuongeza:

“Hakuna tatizo lolote kwenye sheria ya madini. Hata wageni huwa tunakaa nao tunawaelimisha na wanatuelewa vizuri. Kama kuna dosari ni vitu ambavyo tunaweza kuvirekebisha na tayari tumekwishakufanya hivyo kwa baadhi ya maeneo.”

Prof. Msanjila pia aliwashauri viongozi hao kujitangaza zaidi kuhusu kazi zao, huku akiwataka kutafuta wasaa kwa ajili ya pande hizo mbili kukutana ili wizara itoe elimu zaidi kwa jumuiya hiyo kuhusu sekta ya madini zikiwamo fursa za uwekezaji.

Mmoja wa viongozi wa jumuiya hiyo, Francis Nanai ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited, alimweleza Prof. Msanjila kuwa wamezipokea changamoto zilizotolewa kwao ikiwamo ushauri wa kukutana na wizara kwa lengo la kupata ufafanuzi na elimu zaidi kuhusu sekta ya madini.

Habari Kubwa