Utoroshaji mifugo nje ugharimu serikali bilioni 263

17May 2018
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Utoroshaji mifugo nje ugharimu serikali bilioni 263

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema Serikali kila mwaka inapoteza jumla ya sh bilioni 263 kufuatia kushamiri kwa utoroshaji wa mifugo nje ya nchi na uingizaji wa mazao ya mifugo usiozingatia sheria na taratibu za nchi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina kulia akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Longido Daniel Chongolo wakiwa kwenye bango la uzinduzi wa Operesheni Zagamba 2018.

Mpina ameyazungumza hayo jana kwenye mnada wa mifugo wa Namanga wilayani Longido mkoani Arusha wakati wa uzinduzi wa operesheni maalum ya kitaifa ya kudhibiti upotevu wa mapato na usimamizi wa biashara ya mifugo na mazao yake iliyopewa jina la ‘Operesheni Nzagamba 2018’ 

Alisema operesheni hiyo itafika kwenye minada ya mifugo, bandarini, viwanja vya ndege, mipakani, kwenye masoko na maduka, supermarket, na machinjioni ili kujiridhisha na uhalali wa biashara hiyo. Na kwamba operesheni hiyo itamfikia kila mtu anayejishughulisha na tasnia nzima ya mifugo.

Mpina alisema operesheni hiyo imefanikiwa kubaini kuwepo kwa ubabaishaji mkubwa unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kufanya udanganyifu katika biashara ya dawa za mifugo,upotevu mkubwa wa mapato na uingizaji holela wa mazao ya mifugo kutoka nje ya nchi ikiwemo nyama na maziwa kupitia njia za panya.

Akitolea mfano eneo la Namanga zaidi ya mbuzi 22,000 zilikamatwa zikitoroshwa kwenda nchini Kenya huku makusanyo yakiongezeka na kufikia sh milioni 200 kwa muda wa mwezi mmoja tangu kuanza operesheni hiyo ambapo kwa upande wa Mwanza makusanyo yameongezeka kutoka sh milioni 17 kwa mwezi na kufikia Sh. Milioni 532. 

Habari Kubwa