Utouh: Mikopo ya vyuo vikuu ifutwe

04May 2021
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe
Utouh: Mikopo ya vyuo vikuu ifutwe

MWAKA 1994/95, serikali ilianza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na miaka 10 baadaye, yaani mwaka 2004 utoaji wa mikopo hiyo ukachagizwa zaidi na kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Hata hivyo, utoaji wa mikopo hiyo umekumbwa na malalamiko kutoka kwa wadau ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa kile kinachotajwa kuwa uonevu katika marejesho.

Vilevile, zipo hoja za matumizi mabaya ya fedha za bodi hiyo zilizoibuliwa na vyombo vya ukaguzi ikiwamo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kwa kurejea machache, PAC ilibaini mamilioni ya HESLB kutumiwa na maofisa wake kulipana posho mbalimbali ikiwamo ya ukarimu, huku Ripoti mpya CAG ikibainisha wadaiwa sugu 128,278 hawajulikani waliko na wanatakiwa kurejesha Sh. bilioni 706.7 walizokopeshwa.

Wakati hali ikiwa hivyo, aliyekuwa CAG, Ludovick Utouh, anaishauri serikali kuifuta mikopo hiyo.

Katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Utouh alisema anaona kuna haja kuachana na utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa ufanisi umekosekana katika marejesho huku kukiwapo taarifa za uonevu katika kurejesha mikopo hiyo.

Utouh ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WAJIBU, alisema elimu ni miongoni mwa huduma za msingi ambazo serikali inapaswa kuzitoa kwa wananchi wake, hivyo siyo haki wananchi kukopeshwa fedha ili wapate haki yao.

"Niseme tu kwamba mkopo ni pesa ambayo unaipokea ili baadaye uilipe, lakini tulisema tunakopesha watu wasome, waajiriwe na kupitia mshahara wao wa kuajiriwa warudishe deni.

"Sasa tunasomesha watu wanahitimu lakini hawana ajira, ndio maana CAG anasema kuna wadaiwa sugu 128,000 na watu hao wakati mwingine hata kuwapata katika mifumo maalum inakuwa ni shida.

"Kwa hiyo, mimi ninafikiri tunatakiwa kurudia kufikiria yale mawazo ya kukopesha mtu asome, ahitimu, ajiriwe, kupitia mshahara alipe deni.

"Sasa, kwenye hali yetu hii ambayo hakuna ajira, tutawezaje kurudisha gharama hizo? Tufike mahali tufikirie tena hii mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

"Watu wanasoma kupitia mikopo lakini hawajaajiriwa, ni vipi watarudisha? Kuwe na sheria ya kusema kuwa huyo mtu akimaliza masomo yake bila kupata ajira kwa kipindi fulani nini kifanyike, kuliko kuripoti kwenye vitabu kusema bodi ya mikopo inadai kiasi kikubwa wakati tunajua uwezekano wa kurudisha ni sifuri.

"Sisi tuliosoma zamani tulikuwa hatulipi, tulipewa hadi fedha za usafiri (nauli) lakini wakati huo tulikuwa wachache na vyuo vilikuwa vichache.

"Suala la afya, elimu na maji ni jukumu kwa kuwa ndiyo huduma kuu zinazopaswa kutolewa na serikali," Utouh alifafanua.

Takwimu za HESLB za mwaka 2019, zilibainisha kuwa kati ya Watanzania 479,779 waliopatiwa mikopo hiyo tangu serikali ilipoanza kuitoa mwaka 1994/15, ni wanufaika 11,214, sawa na asilimia 2.3 waliofanikiwa kumaliza kulipa madeni yao.

Deni kuongezeka kwa asilimia sita kila mwaka, kumekuwa kukitajwa kuwa kiini cha wanufaika wengi wa mikopo hiyo kushindwa kumaliza kulipa madeni yao.

Katika hotuba yake jijini Mwanza wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi Mei Mosi mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kuifuta 'riba' hiyo iliyolalamikiwa kwa muda mrefu.

Habari Kubwa