Utouh: Vijana washiriki kuandaa bajeti ya serikali

03Oct 2021
Halfani Chusi
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Utouh: Vijana washiriki kuandaa bajeti ya serikali

MKURUGENZI wa Taasisi ya WAJIBU inayojihusisha na masuala ya uwazi na uwajibikaji, Ludovick Utouh, ameshauri vijana washirikishwe katika uaandaji wa bajeti kuanzia ngazi ya chini hadi kitaifa.

MKURUGENZI wa Taasisi ya WAJIBU inayojihusisha na masuala ya uwazi na uwajibikaji, Ludovick Utouh:PICHA NA MTANDAO

Utouh aliyewahi kuwa Mdhibiti ba Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alitoa rai hiyo mkoani Dar es Salaam juzi alipokutana na wananvyuo ambao wapo ndani ya klabu za uwajibikaji na kufanya majadiliano nao juu ya mambo kadhaa ikiwamo uwajibikaji wao katika upangaji wa  bajeti.

Mkurugenzi huyo alisema vijana wengi wamekuwa hawahusishwi katika suala zima la upangaji bajeti kuanzia ngazi ya chini hadi kitaifa.

 Alisema vijana wana nafasi kubwa ya kuiletea nchi maendeleo chanya kama watapewa nafasi ya kushiriki katika upangaji wa bajeti katika ngazi zote ikiwamo serikali za mtaa, kata hadi katika ngazi za kitaifa.

 "Vijana ndio watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii. Maendeleo yao yanaendana na mipango ya bajeti itakayopangwa pamoja lakini pia wana nafasi ya kuelimisha Watanzania wengine ili taifa liweze kisonga mbele," alisema.

Utouh aliongeza juwa mwaka ujao utakuwa wa Sensa ya Watu na Makazi, hivyo vijana bado wana nafasi kubwa ya kuhamasisha watu kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa ili serikali ijue idadi halisi ya watu waliopo nchini ili kuipa nafasi serikali kupanga bajeti kuendana na idadi ya watu waliopo.

Katika hafla hiyo, pia kulikuwa na ugawaji wa zawadi kwa wananvyuo 23 kutoka vyuo mbalimbali walioshiriki katika kuandika insha nzuri iliyohusu njia za kusaidia kuongeza ushiriki wa vijana kwenye uandaaji wa bajeti ya taifa.

 Kati ya hao 23 walioshiriki, Raymond Manyenye kutoka Chuo Kikuu cha Mipango Dodoma, aliibuka mshindi katika kinyanganyiro hicho akifuatiwa na wengine wa nne katika nafasi ya tano bora huku wengine ambao hawakufanikiwa kushinda, wakipongezwa kwa kushiriki kwa kupewa zawadi ya cheti na kitabu kilichondikwa na Ludovickh Utouh,  kinachozungumzia zaidi uwajibikaji kwa vijana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, alisema zaidi asilimia ya watu nchini ni vijana, hivyo kuna kila sababu ya kuwatumia vijana katika kutoa uamuzi.

"Ninashukuru sana kualikwa na WAJIBU, kwangu hii ni heshima kubwa sana, ni jambo muhimu sana hasa tunapoangalia vijana kushiriki, kwa hiyo ni muhimu kama hivi kuwakutanisha vijana na kuwapa elimu.

"Nitoe rai kwa jamiii kupitia vyombo vya habari pale vijana tunapopata nafasi ya kushiriki tushiriki kikamilifu," alisema.

Habari Kubwa