Uuzaji nje kahawa ghafi wapigwa ‘stop’

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
RUVUMA
Nipashe Jumapili
Uuzaji nje kahawa ghafi wapigwa ‘stop’

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amepiga marufuku uuzaji wa kahawa isiyokobolewa nje ya nchi, lengo likiwa kuiongezea thamani kabla ya kuingizwa sokoni.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa

Pia ameziagiza halmashauri zinazolima kahawa nchini kuwa na kitalu chenye zaidi ya miche 200,000 ifikapo mwisho wa Februari, mwaka huu na kuagiza Wizara ya Kilimo kufuatilia utekelezaji huo.

 

Majaliwa aliyasema hayo juzi alipokuwa  akizungumza na wadau wa kahawa wa mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga.

 

Waziri Mkuu alisema kuanzia sasa kahawa yote itakayozalishwa nchini ni lazima iongezewe thamani na hakuna kahawa yenye maganda itakayoruhusiwa kuuzwa nje ya nchi.

 

“Hairuhusiwi kutoa kahawa nchini na kuiuza nje ya nchi ikiwa bado na maganda. Ni  lazima iongezewe thamani ndipo ipelekwe katika masoko ya nje ya nchi ili iuzwe kwa bei nzuri. Hatua hii itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani na kusaidia kulinda uwekezaji wa viwanda uliofanyika nchini,” alisema.

 

Kuhusu madeni ya wakulima, aliagiza watendaji wote wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) waliohusika watafutwe na walipe deni.

 

 “Kwa sasa serikali haina taratibu za kununua madeni ya chama chochote cha ushirika. Kuendelea na utaratibu huo kunachochea viongozi wa ushirika kufuja mali za ushirika. Lazima watambue ukifuja fedha za wanaushirika  serikali iko na wewe,” alisema.

 

Waziri Mkuu alisema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, haitorudi nyuma katika msimamo wake wa kuwasimamia wakulima nchini ili nao wanufaike na kazi kubwa wanazofanya.

 

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa Amcos wahakikishe wakulima wote wanasajiliwa na taarifa zao ikiwamo ukubwa wa mashamba, kiasi cha uzalishaji na mahali walipo zinatunzwa vizuri katika kompyuta.

 

Pia alimwagiza Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Ruvuma, akague Amcos zote na kujiridhisha kama ziko hai na kwenye tatizo la uongozi aitishe uchaguzi.

 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema minada yote ya kahawa itafanyika kwenye maeneo yanayolima ambayo yamegawanywa kwa kanda.

 

Alitaja kanda hizo na mikoa kwenye mabano kuwa ni Moshi (Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara), Kagera (Kigoma, Geita, Kagera na Mara), Songwe (Rukwa, Mbeya, Iringa, Songwe na Katavi) na Mkoa wa Ruvuma utafanyika Mbinga.

 

Alisema lengo ya kufanya minada hiyo katika maeneo yanayolima kahawa ni kuongeza uwazi katika biashara hiyo na kuwawezesha wakulima kujua bei ya mnada na kulipwa kwa wakati. Mkulima anaruhusiwa kupeleka kahawa katika mnada wowote nchini ilimradi azingatie sheria na taratibu husika.

 

“Kila kanda inayolima kahawa nchini itakuwa na maeneo yake ya kuuzia na kahawa ya Mbinga itauzwa katika minada itakayofanyika Mbinga na bei kila mtu ataijua siku hiyo.”

 

 

 

Habari Kubwa