UVCCM yaunga mkono Mramba kutumbuliwa

04Jan 2017
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
UVCCM yaunga mkono Mramba kutumbuliwa

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema umefurahishwa na kitendo cha Rais John Magufuli, kupigania maslahi ya wanyonge na kuzuia upandishaji wa bei ya umeme nchini.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka.

Aidha UVCCM umeelezea kufurahishwa kwao na kuunga mkono uamuzi huo ambao umethibitisha kuwa Rais Magufuli ni mtawala anayejali, kuthamini na kupigania maslahi ya wananchi wanyonge na wenye vipato vya chini.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, wakati wa kikao cha watumishi wa umoja huo kwa ajili ya kutathmini utendaji wa mwaka 2016 na kuweka mikakati ya utendaji kwa mwaka huu.

Shaka alisema kitendo cha Rais Magufuli kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba, ameonyesha ujasiri, uzalendo na upendo kwa wananchi ambao walimpa dhamana ya kuongoza nchi.

“UVCCM tunaunga mkono uamuazi wa Rais wa kuzuia kupanda kwa bei ya umeme na ametazama maslahi ya wananchi waliomchagua kuingia madarakani,” alisema Shaka.

Aidha, alisema Tanesco kupitia Mkurugenzi wake Mramba na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kwa pamoja waliwaahidi wananchi bei ya umeme haitapanda, hivyo kama ingepanda na serikali ikakaa kimya, ingekuwa aibu.

Shaka aliwataka watendaji wa serikali, wakurugenzi wakuu wa mikoa, wajumbe wa bodi makamishna, makatibu wakuu na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, waendelee kutekekeza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu na sheria bila kukurupuka.

“Viongozi wa serikali wanatakiwa kujua mambo yamebadilika kwa ujumla Rais Magufuli na serikali yake ipo makini kwa kufuatilia kila jambo na atakayekwenda kinyume ajiandae kutumbuliwa,” alisema Shaka.

Aidha, alisema UVCCM imewahimiza watendaji na watumishi wa serikali waliopo katika sekta za maendeleo kusoma upepo, kutenda haki, kutimiza wajibu na kupitisha maamuzi kwa maslahi ya nchi.

“Tutaendelea kuipongeza Serikali ya CCM kwa kazi nzuri wanayofanya katika kusimamia nidhamu ya utendaji kazi na tunamshauri Rais Magufuli aendelee kusimamia majukumu yake ili watu wafanye kazi zao kwa kufuata muongozo na taratibu zilizopo za nchi,” alisema Shaka.

Habari Kubwa