Uvunjaji, wizi majumbani Dar washika kasi

21Apr 2022
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uvunjaji, wizi majumbani Dar washika kasi

MATUKIO ya kuvunja madirisha na milango kisha kuiba vitu vya thamani kwenye nyumba pamoja na magari katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam yameanza kushika kasi.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa rai kwa mitaa ambayo haina vikundi vya ulinzi shirikishi vianzishe ili kudhibiti matukio hayo.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, waathirika wa matukio hayo walisema wahalifu hao wamekuwa wakitumia dawa za usingizi kupuliza vyumbani nyakati za usiku wakati watu wamelala ili kutekeleza uhalifu pasipo wahusika kugundua.

Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Mary Mashina, ambaye ni mkazi wa Tabata Segerea Chama, akisimulia alivyoibiwa alisema mwanzoni mwa Machi, mwaka huu, waliamka asubuhi na kukuta wameibiwa baadhi ya vitu vya ndani.

“Siku hiyo watu wote nyumbani tulichelewa kuamka. Tuliamka majira ya saa tatu asubuhi hali ambayo si ya kawaida. Nilipoenda subuleni nikakuta televisheni na redio hakuna na mlango ukiwa umevunjwa. Nikabaini kwamba tumeibiwa. Nikaenda Kituo cha Polisi Stakishari kuripoti,” alisema.

Mkazi mwingine wa Kimara Saranga, maarufu Kwa Makofia, Mayala Mwendesha, aliliambia gazeti hili kuwa juzi usiku aliibiwa gari lenye namba za usajili T 540 DVJ aina ya Probox Succeed lenye rangi ya silver.

Alisema wizi huo ulifanyika usiku baada ya kutoka safarini na familia yake, kisha kuliegesha gari nje na kwamba walipoamka asubuhi hawakukuta gari.

“Nilipata msiba mama yangu alifariki dunia kwa hiyo nilisafiri pamoja na familia yangu kwa kutumia gari hilo ambalo ni mali ya mdogo wangu. Tumerudi nyumbani (Dar es Salaam) jana (juzi) na tulifika majira ya saa nne usiku.

“Ndani ya gari tulikuwa tumeweka vitu mbalimbali vikiwamo vyakula ambavyo tulinunua wakati tunarudi. Baada ya kufika nyumbani niliwaambia wanafamilia vitu hivyo watavishusha kesho (juzi) asubuhi maana wote tulikuwa tumechoka,” alisema.

Alisema kitu ambacho alishuka nacho kwenye gari ni kompyuta mpakato na vingine viliendelea kubaki kwenye gari hilo.

“Ilipofika jana (juzi) asubuhi baada ya kuamka ndipo tulikuta gari halipo. Nyumba yangu imezungusha ukuta isipokuwa eneo la mbele pako wazi sijamaliza ujenzi. Nimetoa taarifa Kituo cha Polisi Gogoni Kiluvya,” alisema.

Mkazi wa Tabata Kinyerezi Mtaa wa Zimbili (jina limehifadhiwa) aliieleza Nipashe kuwa usiku wa kuamkia juzi, alisikia kelele kutoka nyumba ya jirani yake akiomba msaada baada ya kuvamiwa na wezi.

“Wakati jirani yangu akiomba msaada akiita wezi wezi, wale wezi wakatoka nje nikawa nawasikia wakiongea nje ya ukuta wa nyumba ninayoishi wakisema yeyote atakayesogea watamdhuru,” alisema.

Alisema ilipofika asubuhi alibaini kwamba jirani yake aliibiwa televisheni na simu, kisha kujeruhiwa na panga mkononi.

Kijana huyo alisema kabla ya tukio hilo, wiki moja iliyopita mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi wakati akienda kituo cha daladala majira ya saa 12:00 alfajiri, alivamiwa na vibaka kisha kumpora begi lake na kukimbia nalo.

“Hawa vibaka ninadhani walijua ndani ya begi kuna kompyuta mpakato. Sasa  wakati mtoto akipiga kelele za kuomba msaada, wale vibaka walipokimbia mbele walipekua na kukuta lina madaftari, hivyo walilitelekeza njiani,” alisema.

Kutokana na kutokea kwa matukio hayo Nipashe ilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ambaye alikiri kwa baadhi ya maeneo ambayo hayana vikundi vya ulinzi shirikishi yamekuwa yakikumbwa na matukio hayo.

 “Tabata Magengeni, Tabata Kimanga, Mwenge na maeneo mengine tumeshadhibiti. Walipiga kidogo miezi minne iliyopita lakini kwa sasa imebaki hadithi, kazi kubwa imefanyika. Baadhi ya maeneo wako vibaka lakini kazi kubwa inafanywa na Jeshi la Polisi ya kuwadhibiti,” alisema.

Hivyo, alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha maeneo ambayo hayana vikundi vya ulinzi shirikishi vianzishwe ili kudhibiti uhalifu kama walivyofanya maeneo mengineyo.

Habari Kubwa