Uwekezaji bil. 35 kupunguza uhaba saruji

17Apr 2021
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Uwekezaji bil. 35 kupunguza uhaba saruji

KIWANDA cha saruji cha Twiga kinatarajia kuwekeza Dola za Marekani milioni 15 sawa na Sh. bilioni 35 kwa ajili ya kukarabati mitambo na kukiongezea uwezo wa uzalishaji.

Hayo yalisemwa jana na Meneja Biashara Mwandamizi wa Kampuni hiyo, Danford Semwenda, wakati ujumbe wa Kituo cha Uwekezaji Tazania (TIC) ulipotembelea kiwanda hicho kilichoko Wazo, Dar es Salaam.

Ujumbe huo ulitembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kujionea shughuli za uzalishaji na kusikia changamoto mbalimbali ambazo wawekezaji hao wanakabiliana nazo ili wazitatue.

Semwenda alisema wamekuwa na changamoto ya kucheleweshewa shehena ya mizigo yao bandarini hali ambayo husababisha mizigo yao kukaa muda mrefu na kutozwa faini kubwa.

“Uwekezaji unaofanyika hapa ni mkubwa sana hivyo tunahitaji watu kama TIC waje wasikilize kero zetu na kwa kweli tumefurajia ujio wao hapa kwasababu umeonyesha namna gani walivyotayari kutusaidia,” alisema Semwenda.

Aidha, alisema kiwanda hicho kimekuwa kikilipa kodi serikalini zinazofikia Sh. bilioni 54 na kutoa ajira kwa maelfu ya vijana wa Kitanzania. Pia alisema kwenye awamu ya tano, kiwanda hicho kilifanya biashara kubwa ya saruji.

Semwenda alisema miradi ya kimkakati iliyotekelezwa kwenye awamu ya tano ilisababisha saruji kuhitajika kwa wingi hali iliyosababisha wapate faida na kuongeza gawio kwa wanahisa wake kwa asilimia 40.

Bevin Ngenzi, Meneja wa TIC Kanda ya Mashariki,  alisema wameamua kutembelea kiwanda hicho kujua kinavyoendelea na uzalishaji na  kuangalia changomoto wanazokaliana nazo ili waweze kuzitatua.

Alisema TIC imefurahi kusikia kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikiongeza uwezo wake wa kuzalisha kila mwaka hali ambayo imesaidia serikali kupata kodi kubwa na Watanzania wengi kupata ajira.

Ngenzi alisema miaka 10 iliyopita kiwanda hicho kilikuwa kikizalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka na sasa uwezo wake umeongezeka hadi kufikia tani milioni mbili kwa mwaka.

“Wawekezaji hawa wanaendelea vizuri na wameishukuru serikali kwa mazingira mazuri ila kuna changamoto ndogo ndogo za kisera ambazo tunakwenda kuzifanyia kazi haraka,” alisema Ngenzi.

Alisema mwekezaji huyo ameelezea changamoto ya kuchelewesha mizigo bandarini hivyo watakwenda kukaa na taasisi husika kuhakikisha changamoto hiyo inafanyiwa kazi.

Alisema kazi ya TIC ni kuhakikisha wawekezaji wanafanya biashara katika mazingira mazuri na tulivu hivyo wataendelea kutembelea viwanda na kampuni ili kusikiliza kero mbalimbali.

Habari Kubwa