UWT Tabora kupewa mtaji wa mil 41.2 na Jaquiline

11Jul 2021
Halima Ikunji
Tabora
Nipashe Jumapili
UWT Tabora kupewa mtaji wa mil 41.2 na Jaquiline

​​​​​​​MBUNGE wa Viti Maalumu mkoani Tabora kupitia Jumuiya ya Wanawake (UWT) Jaquiline Kainja, ameahidi kuwainua kiuchumi wanawake wa Mkoa huo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata zote 206  kwa kuwawezesha mtaji wa shilingi milioni 41.2 ili kuanzisha miradi ya maendeleo.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora Jaquiline Andrew Kainja, akiongea na wanawake wa Mkoa wa Tabora katika mwendelezo wa ziara yake katika Wilaya zote 7 za mkoa huo. Picha na Halima Ikunji

Ametoa ahadi hiyo katika ziara yake inayoendelea ya kutembelea Wilaya zote 7 za Mkoa huo na kukutana na Wajumbe wa Baraza la Wanawake (UWT) wa kila Wilaya kwa ajili ya kuwashukuru na kuwaeleza nini anachotaka kuwafanyia.

Amesema yeye kama Mbunge anayewakilisha wanawake wote wa Mkoa huo anajukumu kubwa la kuhakikisha wanainuka kiuchumi, hivyo anakusudia kutoa kiasi cha shilingi laki 2 kwa wanawake katika kila Kata ili kuanzisha miradi yao.

Amebainisha kuwa waliompeleka bungeni ni akinamama hivyo kazi yake ni moja tu ya kuwatumikia, kuwasemea na kufanya kila linalowezekana ili kuharakisha maendeleo yao kijamii na kiuchumi.

Kainja amefafanua kuwa wataanza na kata 5 katika kila Wilaya na atashirikiana na madiwani wa viti maalumu ili kuhakikisha wanawake wa kila kata wanafikiwa na mpango huo ili kuwainua kimaisha.

"Nitatembelea kata zote ili kuwashukuru na kwa akinamama ambao hawamfahamu mbunge wao hii ni fursa muhimu ya kumwona, na siku nikija naomba nipate taarifa ya wanachama wapya mliwaingiza UWT’ amesema Kainja.

Aidha Kainja amewataka madiwani wa viti maalumu na kata kufuatilia maendeleo ya vikundi vya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu vilivyoko katika kata zao na kujua changamoto zinazowakabili ili kuzitafutia ufumbuzi.

Katibu wa UWT Mkoani Tabora  Hawa Makoyola amempongeza Jaquiline kwa kuwawakilisha vyema bungeni na kwa dhamira yake njema ya kuwainua akinamama wa mkoa huo kiuchumi, alimhakikishia kuwa wataendelea kumuunga mkono na kumwombea kwa Mungu ili aendelee kuwatetea vyema bungeni.

Naye Katibu wa CCM wilaya ya Uyui Neema Lunga amesema serikali ya CCM ina nia ya dhati kuwainua wanawake wote kimaisha pasipokuangalia itikadi zao, na kubainisha kuwa hata wanawake wote walioteuliwa kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama au serikalini hawatawangusha viongozi wao.

Habari Kubwa