VAT yakwamisha ujenzi wa stendi mpya ya Dar

22Jun 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
VAT yakwamisha ujenzi wa stendi mpya ya Dar

MKURUGENZI wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, amesema ujenzi wa stendi mpya ya kisasa ya mabasi umekwama kutokana na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuwa kubwa.

Muonekano wa stendi mpya ya kisasa ya mabasi utakapokamilika.

Amesema hali hiyo imesababisha vifaa walivyonunua kwa ajili ya kazi hiyo kukwama bandarini.

Liana aliyasema hayo jana mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sulemain Jafo, wakati akitoa maelezo ya mradi huo.

Jafo alifanya ziara ya kukagua ujenzi wa mradi huo pamoja na barabara zilizoko chini ya mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

 "Serikali Kuu ilitupatia Sh. bilioni 50.95 bila VAT Januari 18, mwaka huu na  mkandarasi alianza kazi na mpaka Juni 19, tumepata changamoto ya VAT. Nimekuwa nikifuatilia suala hilo hadi mkoani Dodoma pale Hazina, lakini mpaka sasa nimekwama," alisema.

Alisema wiki iliyopita alijulishwa kwamba kamati imeshakaa na kuidhinisha, hivyo kutokana na ucheleweshaji huo wana wasiwasi kwamba endapo mkandarasi ataruhusiwa kwenda kununua vitu, kuna uwezekano asirudishiwe fedha zake.

"Mheshimiwa Waziri tumesubiri sana tunaomba utusaidie tena katika suala hilo maana tumekwama na changamoto nyingine ilikuwa ya mvua kunyesha ilitusumbua sana, lakini hadi sasa tumefikia asilimia 20 ya kazi hii ya ujenzi. VAT ikishughulikiwa mapema itasaidia hata kumaliza kabla ya muda," alisema.

Waziri Jafo alisema tayari alishamweleza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuhusiana na watu wake kukwama katika ujenzi kutokana na suala la VAT.

"Si kwamba mradi huu tu ndio umekwama. Miradi yote ya DMDP imekwama, nina imani kuwa Dk. Mpango atakwenda kulishughulikia kwani nilishamwambia na nimeandika barua kwa kuwa Rais (John Magufuli) ametoa fedha, hatuko tayari kuona unachelewa huu mradi," alisema Jafo.

 Aidha, Jafo alimtaka mkandarasi anayejenga mradi huo kuongeza kasi katika ujenzi huo na kwamba hataki kusikia kisingizio cha mvua kukwamisha ujenzi huo.

 "Huu mradi mko nyuma kwa asilimia nane, sitaki kusikia mvua mkandarasi kama watu wanajenga baharini ambako kuna maji wewe uanshindwa nini hapa? Mbona baharini wanajenga?" Alihoji.

"Hii miradi ni ya pekee na ndiyo maana Rais John Magufuli aliamua kutoa Sh. bilioni 268.75 haijawahi kutokea ni kwa mara ya kwanza zamani ilikuwa jiji linachukua mikopo kwa benki za kibiashara," alisema.

Alisema Rais Magufuli alitoa Sh. bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi huo wa kituo cha mabasi, hivyo ameridhishwa na utendaji kazi na kuwataka kukamilisha ndani ya muda.

Aidha, alimwagiza mshauri mwelekezi kuhakikisha anasimamia vizuri mradi huo na pasijitokeze kwa dosara ya aina yoyote.

"Ndiyo maana nilikuwa nakuuliza maswali mengi kuhusiana na huu mradi nataka kila kitu uwe unakijua wewe, mkandarasi anaweza kufanya vitu vidogo ili apate faida nataka mambo yaende vizuri hizi Sh. bilioni 50 ni nyingi," alisema.

Alisema stendi hiyo itakuwa kubwa na ya kisasa, hivyo ifikapo Septemba mwakani iwe imekamilika kabla ya kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

"Mimi ninachotaka kabla ya kuingia katika Uchaguzi Mkuu tumuite Rais Magufuli kuja kufungua huu mradi lengo ni Watanzania waje kuona manufaa ya huu mradi," alisema Jafo.

Aidha, Jafo aliagiza kujengwa kwa haraka barabara ya Mbezi Makonde ambayo inaunganishwa na Old Bagamoyo kwani imekuwa ni kero kwa wananchi.

"Hii barabara hadi wataalamu wangu mmeisahau, mmepata tabu kufika nilikuwa nawaangalia tu kwa nini mmenipoteza kufika hapa. Wataalamu wangu msipojua hizo barabara hamuwezi kujua changamoto za wananchi wanazozipata," alisema Jafo.

Habari Kubwa