Vifo, ulemavu kwa watu kumbana Mpina

17May 2018
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Vifo, ulemavu kwa watu kumbana Mpina

KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imetaja hoja nne ambazo imejipanga kumbana nazo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, atakapowasilisha bungeni jijini Dodoma leo bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, ikiwamo wizara yake kusababisha ulemavu na vifo vya watu.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina.

Ratiba ya vikao vya Bunge la Bajeti iliyotolewa na Idara ya Habari na Elimu ya Bunge inaonyesha kuwa kutakuwa na mjadala wa siku mbili bungeni wa makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kuanzia leo.

Akizungumza na Nipashe kwenye Viwanja vya Bunge jijini hapa jana, Naibu Waziri Kivuli wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Immaculate Sware, alisema wamejipanga kuutumia mjadala huo kumbana Waziri Mpina na serikali kwa hoja nne ambazo ni pamoja na operesheni ya kuzuia uvuvi haramu kufanyika pasi na kuzingatia haki za wavuvi na binadamu wengine wanaoishi maeneo ilimofanyika.

Dk. Sware alisema kulikuwa na ukandamizaji mkubwa wa haki za binadamu wakati operesheni hiyo, akieleza kuwa mbali na kuacha umaskini kwa wavuvi,  imesababisha ulemavu na vifo vya watu.

Mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema watautumia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kumkumbusha Waziri Mpina na serikali kwamba wanapaswa kuzingatia misingi ya sheria, haki za binadamu na utu wakati wa kutekeleza operesheni za aina hiyo.

"Operesheni hii imekandamiza sana wavuvi. Serikali inapaswa kushirikisha halmashauri katika kufanya operesheni za aina hii. Wametumia nguvu kubwa mno," alisema Dk. Sware na kuongeza:

"Wamepiga faini kubwa kubwa hadi kwa wenye mabasi, wameonewa kwa kuwatoza faini. Mtu anakamatwa anasafiri kwenye basi akiwa na samaki watatu lakini mwenye basi anatozwa faini kubwa. Huu ni uonevu."

Dk. Sware aliitaja hoja ya pili ambayo wamejipanga kumbana Waziri Mpina leo kuwa ni mkanganyiko uliopo katika utekelezaji wa Sheria ya Uvuvi.

Alisema sheria inaruhusu nyavu za nchi sita na saba lakini kwenye operesheni ya uvuvi haramu iliyofanywa na Waziri Mpina hivi karibuni, wavuvi waliokuwa na nyavu hizo walichomewa vyavu zao na kutozwa faini.

"Zana za wavuvi zimeteketezwa ilhali sheria inaruhusu aina hiyo hiyo ya nyavu, wavuvi sasa wamekaa tu hawana nyavu, serikali yao imezichoma, kinachofuata ni njaa," alisema.

Msomi huyo alisema hoja yao ya tatu ni vikwazo katika leseni za uvuvi, akieleza kuwa leseni hizo zimekuwa kikwazo kwa wavuvi wengi nchini.

Alisema kuwa mvuvi akipewa leseni ya kuvua Kigamboni, kwa mfano, haruhusiwi kuvua Msasani au kwenye eneo jingine lolote ndani ya Dar es Salaam ilhali maeneo hayo yamo ndani ya mkoa mmoja.

"Wizara inashindwa kuelewa kwamba samaki hawana mipaka?" 

Alisema zaidi Dk. Sware: "Leseni ukataji wake una ma

tatizo. Ukiikata Dar huwezi kuvua eneo jingine, maeneo ni yale yale, mkoa ni huo huo lakini anazuiwa. Samaki hawana mipaka. Na hili linawaumiza wavuvi maana kuna wakati unajua kabisa kwamba muda huu samaki wengi watakuwa eneo Fulani, lakini leseni inakuwa kikwazo."

Dk. Sware aliitaja hoja ya nne ya Ukawa kuwa ni zuio la kutumia mitungi ya gesi katika uvuvi, akibainisha kuwa limekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya uvuvi wa kina kirefu nchini.

Alisema kuwa kutokana na zuio hilo, wavuvi sasa hawawezi kuvua bahari kuu kwa kuwa mitungi ya gesi ambayo ni ya lazima katika aina hiyo ya uvuvi, imeharamishwa na serikali kutumika katika uvuvi.

"Lengo la serikali ni kuzuia majongoo bahari, lakini wanaovua majongoo bahari ni wachache mno, kwanini serikali isiwadhibiti tu hao wachache na kuruhusu wavuvi wa kina kirefu waendelee na shughuli zao kwa kutumia hiyo mitungi ya gesi?"