Vigezo ma-DED vyatajwa, mkeka kutolewa karibuni

30Jul 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Vigezo ma-DED vyatajwa, mkeka kutolewa karibuni

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, amesema teuzi wa wakurugenzi wa halmashauri utakaofanywa na Rais utazingatia fedha za maendeleo zilivyotumika kutatua kero za wananchi.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, picha mtandao

Pia amesema baada ya uteuzi huo, atakwenda kupangua wakuu wa idara kwenye mamlaka za serikali za mitaa ambao wamekaa kwa miaka 10.

Ummy aliyasema hayo jana jijini hapa alipokuwa akitoa taarifa ya mapato na matumizi ya ndani ya halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji kwa mwaka 2020/21.

Alisema anataka kuona fedha za miradi ya maendeleo zinatumika kwenye miradi yenye tija na inayogusa moja kwa moja wananchi na sio kugharamia semina, vikao, safari na mambo mengine yasiyogusa wananchi.

“Nataka kusema nitawapima wakurugenzi wa halmashauri na maofisa mipango. Namshukuru Mungu ndani ya muda mfupi ujao, Rais ataachia ule mkeka. Kwa hiyo kazi ya kwanza nitakayowataka wakurugenzi kufanya na nitawapima ni kiasi gani wamepeleka fedha walizokusanya maana fedha hizi wamezichukua kwa wananchi kwenye ushuru wa mazao na huduma. Ni lazima zirudi kwa wananchi kwenye kutatua kero zao,” alisema.

“Moja ya vigezo vikubwa cha mkurugenzi huyo ama ni mzuri au mbaya, ni fedha kiasi gani kimepelekwa kutatua kero za wananchi. Kwenye hili naomba kurudia tena mara ya tatu sitamwonea aibu na kumvumilia mkurugenzi yeyote na ofisa mipango wa halmashauri ambaye hatapeleka fedha walizokusanya kutatua kero za wananchi,” aliongeza.

Alisema halmashauri zinazokusanya zaidi ya Sh. bilioni tano zihakikishe asilimia 10 zinapelekwa kwenye miundombinu ya barabara.

“Mwaka huu nitampima Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma anionyeshe barabara ya kilometa mbili ambayo imejengwa kwa ushuru na kodi za wana Dodoma na wote tunaokuja Dodoma. Hata Jiji la Tanga hawashindwi kujenga angalau kilometa moja ya lami. Hili linawezekana, kwangu kigezo cha kupima utendaji bora wa mkurugenzi yeyote wa halmashauri na maofisa mipango ni kiasi cha fedha kilichopelekwa kutatua kero za wananchi,” alisisitiza.

Aliagiza Halmashauri zihakikishe zinapeleka na kutumia angalau asilimia 40 ya mapato yaliyokusanywa (kwa halmashauri zinazokusanya chini ya Sh.bilioni tano kwa mwaka) na asilimia 60 (kwa halmashauri zinazokusanya zaidi ya Sh. bilioni tano  kwa mwaka) kwenye miradi ya maendeleo ili kutatua kero za wananchi hususan kuboresha huduma za afya, elimu na miundombinu ya barabara.

Pia alizitaka halmashauri kuhakikisha fedha za mapato ya ndani zinatumika kutekeleza na kukamilisha miradi kwa asilimia 100 ili wananchi waone faida za mapato ya ndani na hatimaye kuongeza mwamko wa ulipaji wa kodi na ushuru.

KINARA NA ZILIZOSHIKA MKIA

Waziri huyo alisema Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale imeongoza katika halmashauri zote 184 kwa kukusanya asilimia 163 ya makisio yake huku Jiji la Dar es Salaam likiongoza kwa mapato mengi zaidi kwa kukusanya Sh. bilioni 67.09.

Hata hivyo, alisema Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 102 ya makisio yake ya mwaka huku Jiji la Arusha likishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya asilimia 80.

Kwa upande wa Manispaa, alisema Kahama imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 109 huku Tabora ikishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya asilimia 76.

“Kwa upande wa miji, Njombe imeongoza kwa kukusanya asilimia 131 ya makisio yake ya mwaka wakati Mji wa Ifakara umekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 64.