Vigingi 10 mtihani kwa wateule wapya wa JPM

29Oct 2017
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Vigingi 10 mtihani kwa wateule wapya wa JPM
  • *Yaelezwa wasiposhtuka ‘panga’ linawahusu …

SIKU moja tu baada ya kuapishwa kwa wateule wapya wa Rais John Magufuli kwa nafasi mbalimbali zikiwamo za ubalozi, ukuu wa mikoa na ukatibu wa wizara, imefahamika kuwa wahusika wanakabiliwa na vigingi takribani 10 kuhakikisha kuwa wanadumu katika nafasi hizo au hata kupandishwa zaidi.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe, ukihusisha mahojiano na wachambuzi mbalimbali wa masuala ya uongozi na pia rejea kadhaa za hotuba za Rais Magufuli, umebaini kuwa wote walioteuliwa na kuapishwa juzi wanapaswa kuzingatia yale yote ambayo Magufuli amekuwa akiyahimiza kila mara kwa minajili ya kuleta mabadiliko yenye mwelekeo chanya wa maendeleo kwa Watanzania.

Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa miongoni mwa mambo ambayo wateuliwa wapya yanaweza kuwagharimu na kujikuta wakiondolewa katika nafasi zao kungali mapema ni pamoja na kuwa wabunifu, kusimamia vyema maeneo yao ili yasikumbwe na kashfa za matumizi mabaya ya fedha za umma na pia kuwa wepesi katika kushughulikia kero za wananchi.

Baadhi ya wateule wapya wa Rais Magufuli walioapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam juzi ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima; Mkuu wa Mkoa Manyara, Alexander Mnyeti; Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joackim Wangabo; Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Luhumbi; Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, ambaye anakwenda kuchukua nafasi ya Dk. Binilith Mahenge aliyehamishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Mabalozi ni pamoja na aliyewahi kuwa mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu huku Prof. Mkenda akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

“Hawa walioapishwa baada ya kuteuliwa kwa ajili ya kuwa wakuu wa mikoa, mabalozi na makatibu wakuu wa wizara wanapaswa kuwa makini kwa sababu hivi sasa mambo yamebadilika…hakuna mwenye uhakika wa kudumu katika nafasi za uteuzi endapo hatazingatia yale anayohimiza Rais kila uchao,” mmoja wa wachambuzi aliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki.

Aidha, mwingine aliongeza kuwa kwa kuangalia orodha ya watu waliowahi kupewa nafasi za juu na kuondolewa katika kipindi cha miaka mwili ya serikali ya awamu ya tano, ni ishara tosha kwamba wateule hao wapya na wengine waliopo kwenye nafasi zao wanapaswa kuwa makini kwa sababu kinyume chake, wanaweza wasidumu kwenye nafasi zao.

Ikiwa ni takribani miaka miwili sasa tangu serikasli ya awamu ya tano iingie madarakani, tayari wateule kadhaa wa nafasi za juu wamejikuta wakiondolewa kutokana na sababu mbalimbali za dhahiri na nyingine bila maelezo mengi, bali mabadiliko ya kawaida.

Baadhi ya wateule wa nafasi za juu walioondolewa ndani ya kipindi cha m iaka miwili baada ya kuteuliwa kwao ni pamoja aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga; aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anna Kilangho Malecela.

Wengine walioondolewa ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo; aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe; aliyekuwa Waziri wa Maji, Gerson Lwenge; aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu; aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana.

VIGINGI 10 MTIHANI

Wakati akiwaapisha jana, Rais Magufuli aliwakumbusha wateule wapya kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi na pia kuhakikisha kuwa wanalenga kuwasaidia wananchi maskini.

Mbali na hayo, baadhi ya mambo yanayoelezwa kuwa yanapaswa kuzingatiwa na wateule wapya wa nafasi za ukuu wa mikoa ili wadumu kwenye nafasi zao au kupandishwa vyeo ni mosi; kuhakikisha kuwa njaa haiweki kambi wkenye maenei yao.

Katika hotuba zake mbalimbali, Rais Magufuli amekuwa akihimiza juu ya umuhimu wa kilimo kwa ajili ya chakula na baishara na kwamba, Mkuu wa Mkoa ambaye Mkoa wake utakumbwa na njaa ajiandae kutumbuliwa kwasababu atakuwa ameshindwa kazi aliyomtuma. Jambo la pili linalopaswa kuzingatiwa ni ubunifu.

Hata wakati akiwaapisha wateule wapya, Rais Magufuli alihimiza juu ya suala hilo kwa kuwataka wateule hao wakawe wabunifu kwa ajili ya kupeleka maendeleo kwenye ameneo yao.

Kigingi cha tatu kwa watakaojisahau, ni kusimamia ukuzaji uchumi kwenye maeneo yao, kwa kuainisha fursa zilizopo na kuvutia wawekezaji wa maeneo mbalimbali yakiwamo ya viwanda.

Kigingi cha nne ambacho ni mtihani kwa wateule hao wapya ni kuhakikisha kuwa maeneo yao hayakumbwi na migogoro isiyokwisha baina ya wakulima na wafugaji ambayo mwishowe husababisha mapigano.

Wateule hao wapya wa mikoa pia wanapaswa kuzingatia kigingi cha tano ambacho ni kumaliza tatizo la uhaba wa madawati kwenye maeneo yao.

Rais amewahi kulisitiza kwa kina jambo hili wakati akihutubia wananchi kwenye sherehe za kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Singida.

Kigingi cha sita, ni kusimamia ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa kwa bei nafuu. Jmabo hili alilisisitiza katika ziara zake za kikazi mkoani Tanga hivi karibuni na kumsifu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert kwa kazi nzuri kabla juzi kumpandisha na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Changamoto ya saba kwa wateule wapya, nis suala la amani na utulivu kwenye maeneo yao. Maandamano na vurugu vyaweza kuwa chanzo cha kutumbuliwa siku moja na hivyo wanapawa kuwa makini katika eneo hilo.

Jambo la nane muhimu, ni kwa wateule hao wapya kuzingatia nidhamu kwa kujiepusha na matendo yasiyolingana na maadili ya nafasi zao, ikiwamo kujihusisha na ulevi.

Hivi karibuni alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa 33  wa mwaka wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT), Rais Magufuli alisema ana ataarifa za wateule wake wanne ambao ni walevi na aliwataka wajirekebishe kabla hajawatumbua.

Jambo la tisa linaoweza kuwa kikwazo kwa kwa wasiokuwa makini miongoni mwao ni kujiweka mbali na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa akitangaza vuita isiyokoma dhidi ya viotendo hivyo na wka sababu hiyo, yeyote asiyekuwa makini atajikuta akipoteza nafasi yake

. Jambo la 10, ni kwa kila mmoja wao kusimamia kwa ukamilifu maelekezo mbalimbali ya serikali, ikiwamo kutoruhusu maeneo yao kuwa chanzo cha kuwapo kwa watumishi hewa na wenye vyeti hewa vya elimu na taaluma.

WASOMI WANENA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ali, alisema endapo wakuu wa mikoa watakwenda kwenye mikoa yao na kufanya kazi kwa mabavu bila kushirikiana na watendaji wa chini yao, ni wzi kwamba wataishia kutumbuliwa.

“Rais Magufuli amewataka wamalize njaa, tatizo la madawati na upungufu wa madarasa lakini haya yote yatafanikiwa ikiwa wakuu wa mikoa watajishusha, watakuwa waadilifu na watii na kushirikiana na madiwani na viongozi wa serikali za mitaa,” alisema.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk. Benson Bana, alisema wakuu wa mikoa ni macho ya Rais na hivyo, wanatakiwa kuwa wabunifu kwenye maeneo yao ili kufanikisha maendeleo.

“Wapo wakuu wa mikoa wameendelea kubaki kwenye nafasi zao kwa sababu wanaonekana ni wabunifu wanatumia rasilimali zinazopatikana kwenye maeneo yao kutimiza azma ya Rais ya kuipelekea nchi kwenye maendeleo, hawa wawe wabunifu kama alivyowataka la sivyo wataishia kutumbuliwa” alisema.  

Habari Kubwa