Vigingi sita kwa mrithi  wa Mukandala UDSM 

07Dec 2017
Sanula Athanas
Nipashe
Vigingi sita kwa mrithi  wa Mukandala UDSM 

PROFESA William Anangisye, leo anakaribishwa rasmi katika cheo kipya cha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) huku zikibainika changamoto sita ambazo anatakiwa kuzitafutia ufumbuzi wakati wa uongozi wake.

Makamu Mkuu mpya wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Willium Anangisye

Juzi, uongozi wa juu wa UDSM ulitangaza mbobezi huyo katika masuala ya elimu ameteuliwa na Mkuu wa chuo hicho, Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete, kushika nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Prof. Rwekaza Mukandala ambaye uongozi wake wa miaka 11 ulifika kikomo Jumatatu.

Oktoba 16, mwaka huu, Prof. Mukandala, katika mahojiano maalum na Nipashe chuoni hapo, mbali na mambo mengine alianisha changamoto kadhaa zilizoukabili uongozi wake ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi, upungufu wa hosteli na wanataaluma. 

Katika mahojiano hayo, Prof. Mukandala alisema ujenzi wa hosteli mpya za Rais John Magufuli umepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya malazi kwa wanafunzi wa chuo hicho.

Hata hivyo, msomi huyo alisema kunahitajika kufanyika ukarabati wa baadhi ya hosteli zake likiwamo jengo la Hall 2 ambalo sasa halitumiki kutokana na miundombinu yake kuchakaa.

Alisema chuo hicho sasa kina hosteli zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 14,200 kati ya 16,000 kilionao.

WAHADHIRI

Katika mahojiano hayo, Prof. Mukandala alisema UDSM ina wanataaluma wapatao 1,300, lakini changamoto iliyopo ni kwamba si wote wana mafunzo ya ngazi ya uzamivu (Ph.D), hivyo mrithi wake anapaswa kujipanga kuhakikisha juhudi zilizoanzishwa na chuo kuwasomesha, zinafanikiwa.

"Kuna baadhi ya nyanja kunakuwa na upungufu wa wahadhiri, hivyo tumeiomba serikali na ombi letu limekubalika hivyo tutaajiri katika nyanja zenye upungufu," Prof. Mukandala alisema siku hiyo.

Aliongeza: "Tatizo kubwa wahadhiri wetu hawana shahada za uzamili na uzamivu. Kwa  sasa hivi wafanyakazi wetu wenye Ph.D wanafika 650 hadi 700, wengine ndiyo wapo katika ngazi za kusoma ili wafikie ngazi hiyo ya Ph.D."

UBORA WA ELIMU 

Prof. Anangisye pia anatakiwa kuangalia ubora wa elimu ikizingatiwa kwamba UDSM ndicho chuo kikuu kikongwe zaidi nchini.

Katika mahojiano na Nipashe, Prof. Mukandala alishauri kuufanyia maboresho mfumo wa elimu nchini akirejea hotuba ya Rais Magufuli ya Oktoba 14, mwaka huu visiwani Zanzibar juu ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, akisisitiza kuwa ipo haja elimu ya Tanzania irejeshwe kwenye misingi ya ujamaa na kujitegemea. 

"Tunapaswa tutengeneze vijana watakaoipigania nchi, kuweza kuwa na uwezo wa wao wenyewe wa kufanya kazi na kuwa na uwezo wa kujitegemea, Ikisimikwa na misingi mingine, pia elimu isukwe vizuri, kama huko nyuma tulikuwa tunasoma huku tumeshika jembe," Prof. Mukandala alisema.

WAPATAO MAJANGA

Prof. Anangisye pia anatakiwa kutekeleza mpango ulioanzishwa na mtangulizi wake kwa kushirikiana na baraza la chuo -- kusomesha wanafunzi wanaopatwa na majanga ya kufiwa na wazazi au wategemezi wao wakati wakiendelea na masomo huku wakiwa hawajapata mikopo ya elimu ya juu.

“Kunakuwa na wanafunzi wanakuwa na shida sana, labda alikuja anajitegemea, wazazi wake ghafla wanakufa, chuo kupitia baraza lake kimekuwa na utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi hao wachache wenye shida kubwa ya kujikimu," Prof. Mukandala alisema siku hiyo.

USUMBUFU MIKOPO

Prof. Anangisye pia anapaswa kujipanga kukabiliana na maandamano ya wanafunzi kutokana na usumbufu katika kupata mikopo na fedha zitokanazo na mikopo hiyo.

Mwaka huu wa fedha serikali imetoa fedha mwezi mmoja kabla ya vyuo kufunguliwa na kuepusha kutokea kwa maandamano ya wanafunzi yaliyokuwa yamezoeleka miaka ya nyuma.

Katika mahojiano na Nipashe siku hiyo, Prof. Mukandala alibainisha kuwa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ndiyo ilikuwa changamoto namba moja kwenye uongozi wake chuoni hapo.

MKATABA TATA 

Prof. Anangisye pia anatakiwa kuhakikisha mkataba wa mradi wa Mlimani City unatekelezwa na kuwa na manufaa kwa UDSM.

Katika ripoti yake ya mwaka wa fedha 2015/16 aliyoikabidhi kwa Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 27, mwaka huu na baadaye kuiwasilisha bungeni Aprili 13, mwaka huu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alibainisha kuwapo kwa dosari nyingi kwenye mkataba wa mradi wa Mlimani City.

CAG Prof. Mussa Assad, mbali na mambo mengine, alibainisha kwenye ripoti yake hiyo kuwa mkataba hauinufaishi UDSM na kulipaswa kuwa kumejengwa hoteli ya nyota tatu hadi kufikia mwaka jana kwenye mradi huo lakini haijajengwa hadi leo.

Prof. Assad pia alibainisha kuwa katika mradi huo ulioanza Oktoba Mosi, 2004, kuna hatari UDSM kupoteza kiasi kikubwa cha mapato ya mradi huo kutokana na ukiukwaji wa mkataba.

CAG pia alisema katika mapitio ya mkataba huo, aligundua hauelezei hali halisi ya ugawanaji mali pindi mkataba utakapoisha (miaka 50 au 85 kutokana na makubaliano ya pande mbili), akibainisha kuwa hakuna makubaliano yoyote yanayoelezea mgawanyo wa mali na miondombinu itakayokuwapo wakati mkataba unaisha.

Kwa mujibu wa Prof. Mukandala, hafla ya kumkaribisha Prof. Anangisye inafanyika kwenye Ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo leo kuanzia saa 7:30 mchana. 

Habari Kubwa