Vigogo maji wajikita Misungwi kumaliza changamoto mradi wa maji

04Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
Vigogo maji wajikita Misungwi kumaliza changamoto mradi wa maji

UONGOZI wa Wizara ya Maji ukiongozwa na Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga pamoja na wataalam wa wizara ya maji wameweka kambi wilayani Misungwi mkoani Mwanza kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa mradi wa maji Mbalika.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akikagua Mradi wa Maji wa Misungwi, mkoani Mwanza.

Hatua hiyo imekuja baada ya utekelezaji wa mradi huo kukwama kutokana na kuchelewa kufika kwa mabomba ya chuma (steel pipes) kutoka kiwandani, jambo lililomlazimu Naibu Waziri Aweso kuitisha kikao cha dharura kitakachofanyika leo tarehe 04 Desemba, 2019 kitakachohusisha Kiwanda cha Tanzania Steel Pipe (TSP), wasimamizi wa mradi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na Mkandarasi wa Kampuni ya Shanxi Construction Engineering Corporation ya China lengo likiwa ni kupata muafaka mradi ukamilike.

Aweso amesema hataondoka wilayani humo mpaka atakapo hakikisha fedha za ununuzi wa mabomba hayo zimelipwa ili kazi ya ulazaji wa mabomba na kazi zote zilizobaki sawa na asilimia 29 ziishe. Nakutoa agizo kuwa mradi uwe umekamilika ifikapo mwezi Machi, 2020 na kuhudumia watu zaidi ya 81,800 katika vijiji vya Nyang’homango, Isesa, Igenge na Mbalika.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akisoma flow meter ya maji katika mtambo wa kusukumia maji katika Mradi wa Maji wa Maji wa Misungwi, mkoani Mwanza.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Aweso ameridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Misungwi uliokuwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), ambao ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99 na kugharimu kiasi cha Shilingi bilioni 12.

Akitoa pongezi kwa MWAUWASA kwa kuhakikisha mradi huo unakamilika kulingana na maelekezo ya mkataba na kuzingatia viwango vya ubora, wakidhihirisha uwezo mkubwa walionao wataalam wa ndani kwa kazi nzuri iliyofanyika.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga aliyekuwa akitoa maelezo kuhusu Mradi wa Maji uliopo katika Chuo cha Ukiliguru, mkoani Mwanza.

Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga ameishukuru sana Serikali kwa kutoa fedha kwa wakati, pamoja na usimamizi mzuri jambo lililosababisha mradi huo kukamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachoakisi thamani halisi ya fedha zilizotumika.

Alisema mradi huo utamaliza kero ya maji ya mji wa Misungwi na kutoa huduma ya majisafi na salama kwa wakazi 64,000 waishio katika mji mdogo wa Misungwi, vijiji vya Nyahiti, Mapilinga na Mwambola mpaka kufikia mwaka 2032.

 

 

 

 

 

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akisikiliza maelezo kutoka Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele (kushoto) wakati akikagua Mradi wa Maji wa Maji wa Misungwi, mkoani Mwanza.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema Mradi wa Maji wa Misungwi ni miongoni mwa miradi mingi ya mfano iliyotekelezwa na Serikali katika mkoa wa Mwanza baadhi ikiwemo Magu, Lamadi na mradi wa mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka (Simplified Sewarage System) ulijoengwa kwa majaribio kwenye maeneo matatu yaliyopo milimani ya Kilimahewa, Mabatini na Igogo katika Jiji la Mwanza.

Akisema kuwa hii inadhihirisha kazi kubwa inayofanywa katika Awamu ya Tano katika kuhakikisha Sekta ya Maji inakua kwa kasi ya kuridhisha na kufanikisha lengo la kufikia uchumi wa kati.

Sehemu ya Mradi wa Maji wa Misungwi inayopokea maji (raw water) na kuyachuja kabla ya kwenda kutibiwa, mkoani Mwanza.

Habari Kubwa