Vigogo 40 matatani kujenga ufukweni

23Nov 2020
Sanula Athanas
Mwanza
Nipashe Jumapili
Vigogo 40 matatani kujenga ufukweni

BAADHI ya matajiri wa Kanda ya Ziwa, wameingia matatani kutokana na kujenga majengo ya kifahari kwenye fukwe za Ziwa Victoria, Nipashe inaripoti kutoka Mwanza.

Katika semina maalum kwa wahariri juu ya Ushiriki wa Vyombo vya Habari Kuhusu Usimamizi wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Ziwa Victoria iliyofanyika jijini Mwanza juzi, uongozi wa Bodi ya Maji katika bonde hilo ilifichua kuwapo kwa dosari ya vigogo hao kujenga nyumba za mabilioni ya shilingi kwenye fukwe hizo.

Ogoma Mangasa, Mkuu wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini wa bodi hiyo, alisema tayari uongozi wa bodi umeandika barua kwa vigogo hao kuzuia maendeleo ya uwekezaji kwenye eneo hilo ili kulinda usalama ziwa hilo.

"Vigogo zaidi ya 40 hadi sasa tumewaandikia barua kuhusu suala hili. Wako katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita," alibainisha Mangasa.

Hata hivyo, kiongozi huyo alianika ugumu unaowakabili katika kutekeleza majukumu yao ikiwamo kuwadhibiti vigogo hao wanaovamia na kuendeleza maeneo ya Ziwa Victoria, akiwataja wanasiasa kuwa sehemu ya mzizi wa matatizo. 

Kiongozi huyo pia alisema uvamizi wa maeneo hayo ya ziwa unachochewa na baadhi ya mamlaka za serikali kutoa vibali vya ujenzi kwenye maeneo hayo ambayo kisheria hayaruhusiwi kuendelezwa.

"Baada tu ya kuwa tumeandika hizo barua, kelele nyingi zimepigwa kwa sababu ukigusa tu suala la maji na ulinzi wa vyanzo vyake, tayari unamtekenya kila mtu.

"Lakini wengi wameitikia wito akiwamo Mzee... (alimtaja mmoja wa mabilionea jijini hapa). Ambao hawajaitikia ni wale ambao wana 'legal documents' (nyaraka za kisheria) kutoka mamlaka zingine za serikali. 

"Tumefanya kazi kwa karibu na NEMC (Baraza la Taifa la Uhifadhi Mazingira) lakini tumepata shida kidogo na watu wa ardhi kutoka Jiji. Wametoa vibali vya ujenzi kwenye maeneo ambayo kisheria hayaruhusiwi kuendelezwa. Wao wamejali zaidi mapato ya jiji. 

"Mpaka sasa, sisi hatujashindwa, tuko katika mazungumzo na hizo mamlaka zingine za serikali. Tukishindwa, tutaliwasilisha suala hili kwa Katibu Mkuu wa wizara ili lishughulikiwe na mamlaka za juu zaidi. Tunatafuta namna bora ili tusiumize upande wowote maana kuna hao waliopewa vibali na mamlaka za serikali, ukikurupuka kutoa uamuzi, unaweza kuitia hasara kubwa serikali," Mangasa alifafanua.

Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya Mwaka 2009, inapiga marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji.

Alisema ujenzi huo holela pia umekuwa chanzo cha mafuriko katika Jiji la Mwanza, yakiwamo yaliyotokea mwezi huu jijini. 

Katika semina hiyo, Mangasa pia alizungumzia tatizo la uchimbaji holela wa visima vya maji, alibainisha kuwa linasababishwa na kukosekana kwa elimu ya uhifadhi na matumizi ya vyanzo vya maji.

"Tumeona pia kwamba faini ni ndogo. Mtu anachimba kisima kwa malipo ya Sh. milioni mbili bila kuwa na kibali. Mkimkamata analipa faini ya laki tano (Sh. 500,000). 

"Tumeona dosari hii, sasa tunafikiri tuanze kuchukua ile adhabu nyingine ya kifungo cha miezi sita gerezani," Mangasa alionya.

Alisema uchunguzi wao umebaini bonde lao lina watumiaji wa vyanzo vya maji 3,934 wanaopaswa kusajiliwa, lakini ni 880 tu (asilimia 22.34) waliosajiliwa, hivyo kuikosesha bodi mapato.

Licha ya kikwazo hicho, Mangasa alisema mapato ya bodi yameongezeka kutoka wastani wa Sh. milioni 600 kwa mwaka (mwaka 2017) hadi Sh. bilioni nne kwa mwaka kwa sasa.

Habari Kubwa