Vigogo Chadema kuanza kujitetea wenyewe

19Oct 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Vigogo Chadema kuanza kujitetea wenyewe

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imekubali pingamizi la Jamhuri kwamba vigogo tisa akiwamo Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuanza kujitetea wao wenyewe kabla ya mashahidi kutoka nje katika kesi inayowakabili dhidi ya uchochezi.

Uamuzi huo ulitolewa jana na mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Hakimu alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote pamoja na vifungu vya sheria vilivyowasilishwa, mahakama yake imeona pingamizi la awali la Jamhuri lilikuwa na mashiko ya kisheria.

Alisema mahakama yake iliwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu na matakwa ya sheria yanaelekeza mshtakiwa kuanza kujitetea dhidi ya mashtaka yake ikiwamo kusomewa upya mashtaka na kumpatia haki zake.

"Mahakama hii baada ya kupitia hoja za pande zote mbili imekubaliana na pingamizi la awali la Jamhuri kwamba kisheria washtakiwa wanatakiwa kuanza kujitetea na mashahidi wao watafuata kutoa ushahidi wao dhidi ya Jamhuri," alisema Hakimu Simba wakati akitoa uamuzi huo mdogo.

Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, alidai wamekubaliana na uamuzi wa mahakama, lakini wanaomba muda wa kutosha wa kuwaandaa washtakiwa hao.

Alidai washtakiwa wote tisa watajitetea na kwamba wameandika barua kuomba vielelezo vinne ikiwamo CD ya video inayoonyesha picha za tukio la maandamano, lakini mpaka sasa hawajapata.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 21, mwaka huu, kwa ajili ya kutoa uamuzi kama washtakiwa wapewe wiki tatu za kujiandaa kutoa ushahidi au la.

Mbali ya Mbowe, washtakiwa wengine ni, Katibu Mkuu Taifa, Dk. Vicent Mashinji, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Katibu Mkuu Taifa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche, Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Wengine ni, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13 likiwamo la kula njama, wote wanadaiwa kuwa, Februari mosi na 16, mwaka jana, jijini Dar es Salaam, walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Habari Kubwa