Vigogo Kitanzini

19Sep 2021
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Vigogo Kitanzini

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa mwezi mmoja kwa viongozi wa serikali kutatua mgogoro wa wananchi wanaodaiwa kuvamia katika eneo la uwanja wa ndege mkoani Mtwara.

Agizo hilo lilitolewa jana mkoani hapa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, alipofanya ziara kwenye uwanja mpya wa ndege Mtwara na kuzungumza na abiria walioshuka ikiwa ni mara ya kwanza kutua kwa ndege katika uwanja huo.

Alisema mgogoro huo ni wa siku nyingi na tayari Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo kwa wahusika kutatua mgogoro huo lakini hadi sasa tatizo halijatatuliwa.

Shaka alisema masuala ya msingi ambayo yanawagusa wananchi wakati umefika wa kuyatatua kwa wakati badala ya kuisababishia serikali hasara.

“Tunapokuwa na changamoto kama hizi ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja, kipaumbele cha kwanza kwa serikali ni kuona namna gani ya kutatua kwa wakati, kama mngeutatua hili tatizo ina maana hata mimi nisingekuta huu mgogoro,” alisema.

Shaka alisema ifike wakati serikali kuheshimu viongozi wao, akifafanua kuwa aliyepita katika eneo hilo na kupewa malalamiko ya mgogoro huo alikuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais ambaye kwa sasa ni Rais Samia.

Alisema Rais alitoa maelekezo kuwa wizara sita wakutane na kutatua mgogoro huo na hadi sasa maagizo yake hayajatekelezwa na mwaka umepita, akisisitiza kuwa sio jambo la busara.

“Maelekezo ya chama tunatoa mwezi mmoja mgogoro huu uishe, mamlaka zote zipo hapa za serikali. Hakuna ugumu katika kutatua huu mgogoro, kuja kwangu mmeweza kumaliza nusu ya mgogoro na haya niliyoyaelekeza nitayafikisha kwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo,” alisema.

Shaka alisema kuwa baada ya mwezi mmoja endapo yasipotekelezwa, watalifikisha kwa Mwenyekiti wao wa CCM na watampatia ushauri wao nini cha kufanyika ili wananchi hao waishi kwa amani.

Aidha, Shaka alisema Kamishna wa Ardhi amedai wameikosesha serikali mapato kutokana na mgogoro huo, fedha ambazo zingesaidia kusukuma gurudumu la maendeleo katika nchi.

“Tunalea migogoro upande mmoja tunakutana wenyewe na upande wa pili tunahujumu nchi wenyewe kwa wenyewe, hatuwezi kwenda kwa ‘style’ hiyo.

"Ifike mahali tuwe na uamuzi sahihi kama eneo hili ni la mamlaka ya viwanja vya ndege basi ijulikane hivyo, kama wananchi wanastaili kupatiwa haki yao wapatiwe, mbona hakuna jambo kubwa huu mgogoro ni mwepesi,” alisema Shaka.

Alisema kwa maelezo aliyoanza kusikiliza juzi na jana kuhusiana na mgogoro huo hata huo mwezi mmoja aliowapatia anaona ni muda mrefu kwa sababu vielelezo vyote vipo.

“Historia ya hili eneo mnalo na inajulikana mnakwepana, mwingine anaingilia huku na mwingine anapenya huku, tunataka kero za wananchi zimalizwe kwa wakati,” aliagiza.

Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hassan Mtenga, alisema wananchi wameanza kuisha kwa siku nyingi katika eneo hilo na lipo kanisa limejengwa tangu mwaka 1953 na sio kweli kuwa wamevamia.

Alisema mamlaka yenye dhamana ya viwanja vya ndege ina eneo lingine ambalo ni pori kubwa, hivyo waangalie namna ya kuwasaidia wananchi hao wasiondolewe.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Julius Ndyamukama, amekubali kutoa kipande cha ardhi kilichovamiwa na wananchi katika eneo la Mtaa wa Mangamba, Kata ya Mtawanya, Manispaa ya Mtwara. 

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya, alisema wanakwenda kufanyia kazi maelekezo waliyopatiwa na tayari amemwagiza Kamisha wa Ardhi kupima maeneo.