Vigogo Tucta wasimamishwa kazi

19Oct 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Vigogo Tucta wasimamishwa kazi

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limewasimamisha kazi Katibu Mkuu wake, Dk. Yahya Msigwa na Naibu wake, Jones Majura, kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka ikiwamo kuuza nyumba.

Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya, picha mtandao

Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya, akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, alithibitisha kusimamishwa kazi kwa watendaji hao wakuu ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

"Wamesimamishwa kazi kwa lengo la kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili, kikao cha kamati ya utendaji kiliwataka kukaa pembeni," alisema Nyamhokya.

"Tumewasimamisha kazi kwa muda ili kupisha uchunguzi na kuona hatua zinazofuata na hatujawafukuza," alisisitiza.

Alipoulizwa kuhusu tuhuma zinazowakabili alisema: "Hayo ni mambo ya kikao cha ndani ni masuala la kamati ya utendaji ya shirikisho, tuhuma zikibainika ndipo tutawajulisha ila ni mambo ya ndani."

Taarifa za awali zilizolifikia gazeti hili zilisema viongozi hao walisimamishwa kazi wiki iliyopita ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili ikiwamo kuuza nyumba ya shirikisho iliyoko Mafinga mkoani Iringa.

Nyamhokya alisema viongozi hao wanadaiwa kuuza nyumba hiyo bila uamuzi wa vikao halali vya shirikisho na bila kufanya tathmini ya jengo lenyewe.

Taarifa za uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo, kwa mujibu wa taarifa za ndani za Tucta, zitapelekwa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu utakaofanyika baadaye mwezi huu ili kutoa uamizi.

"Vikao vitakavyofanyika ndivyo vitaamua hatima yao kama warudishwe kazi au wafukuzwe kabisa," kilieleza chanzo hicho.

Habari Kubwa