Vigogo ununuzi waingia matatani

11Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Mkalama
Nipashe
Vigogo ununuzi waingia matatani

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa, amemwagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Mkalama, kuchunguza utendaji wa kitengo cha ununuzi cha wilaya hiyo kutokana na utekelezaji mbovu wa miradi ya maendeleo.

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa, picha mtandao

Agizo hilo alilitoa jana wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo.

“Nataka Takukuru mkichunguze kitengo cha ununuzi cha Wilaya ya Mkalama kwa sababu nimebaini kuna mwenendo mbaya katika utekelezaji wa miradi hapa wilayani," aliagiza.

Mwanjelwa alidai kitengo hicho kimekuwa kikitoa zabuni za miradi mbalimbali bila kufuata utaratibu ikijumuisha pia upotevu wa vifaa vya ujenzi katika mazingira ya kutatanisha.

Alisema serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha inafikisha huduma karibu na wananchi, akitolea mfano ujenzi wa hospitali, upanuzi wa vituo vya afya na ujenzi wa masoko, lakini wako baadhi ya watumishi wake wanaofanya ubadhirifu.

“Natoa onyo kwa watumishi ambao bado wanafikiria kujipatia fedha kupitia miradi hii na ninawapa pole kwa sababu serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Magufuli haitaki mzaha katika utendaji kazi," alitahadharisha.

Alisema serikali inataka watumishi walio safi kiutendaji, wanaowajibika ipasavyo na wanaofanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za kiutumishi.

Katika hatua nyingine, Mwanjelwa amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kutekeleza agizo la serikali la kuwaondoa kazini watumishi wenye vyeti vya kughushi.

Maelekezo hayo aliyatoa baada ya kupokea malalamiko ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Malela, Alfred Panda, aliyetaka kujua hatima ya mmoja wa walimu wake aliyebainika kuwa na cheti cha kughushi wakati wa kusafisha taarifa za watumishi, lakini amekuwa akiendelea na kazi na amefuatilia barua yake ya kusimamishwa kazi bila mafanikio.

Mwanjelwa alimtaka mkurugenzi huyo kulifanyia kazi suala la mtumishi huyo haraka iwezekanavyo.

“Mkurugenzi hakikisha hatua kali za kisheria zinachukuliwa haraka kwa mtumishi huyu ambaye ana vyeti feki na unipe mrejesho," aliagiza.

Naibu Waziri huyo yuko mkoani Singida kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na kukutana na watumishi ili kusikiliza kero zao na kuzitatua.

Habari Kubwa