Vigogo viwanda vilivyobinafsishwa wanukia Mahakama ya Mafisadi

15May 2019
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Vigogo viwanda vilivyobinafsishwa wanukia Mahakama ya Mafisadi

SERIKALI imetangaza kuwachukulia hatua kali za kisheria wawekezaji waliobinafsishiwa viwanda kisha kuvichukulia mikopo mikubwa benki na kushindwa kulipa.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda.

Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma jana, hotuba ya makadirio kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, aliwataka wawekezaji hao kuhakikisha wanamalizana na benki walikochukua mikopo kufikia Mei 31, mwaka huu.

Alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaokaidi agizo hilo la serikali kwa kuwa kwa kuchukua mikopo hiyo mikubwa walitenda kosa la uhujumu uchumi, hivyo kuwa hatarini kufikishwa kwenye Mahakama ya Mafisadi.

"Nachukua nafasi hii kuwatahadharisha wahusika wote walioko ndani na nje ya nchi kwamba kwa kufanya hivyo walitenda kosa la uhujumu uchumi. Nawaonya kwamba wahakikishe wamemalizana na mabenki kwa kulipa mikopo yao yote ifikapo Mei 31, mwaka huu," alisema.

Kakunda aliongeza kuwa serikali haitaongeza muda ambao walipaswa kuleta maelezo yenye kueleweka serikalini kuhusu viwanda hivyo.

Kakunda alibainisha kuwa kati ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa, 88 vinafanya kazi huku 68 vikiwa havifanyi kazi.

Alisema kati ya viwanda 88 vinavyofanya kazi, 42 vinafanya kazi vizuri sana, 46 vinafanya kazi kwa kiasi cha kuridhisha na 20 vimefutwa kwa sababu ubinafsishwaji wake ulifanywa kwa kuuza mali moja moja na vingine kuruhusiwa kubadili matumizi.

"Viwanda vingine 48 wamiliki wameshindwa kuviendesha kwa mujibu wa mkataba wa mauziano na hivi sasa, tayari viwanda 16 vimerejeshwa serikalini na vingine 32 wamepewa notisi ya kuwasilisha mipango ya kuviendeleza kabla ya Mei 31, mwaka huu," alisema.

Aliongeza kuwa viwanda 13 havikubinafsishwa kutokana na sababu mbalimbali na hivyo kuendelea kuwa mali ya umma chini ya Msajili wa Hazina. Pia  alisema baadhi ya viwanda hivyo vinafanya kazi kwa kusuasua na vingine havifanyi kazi.

Habari Kubwa