Vigogo wa CHADEMA Ubungo watua ACT

15Jul 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Vigogo wa CHADEMA Ubungo watua ACT

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepata pigo baada ya baadhi ya wanachama wake akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Ubungo, Renatus Pamba, kuhamia Chama cha ACT-Wazalendo.

Imedaiwa kuwa, chanzo cha wanachama hao kukihama chama hicho kikuu cha upinzani nchini, ni kile wanachoona ukiukwaji wa Katiba ya chama hicho baada ya kuwavua uongozi.

Akizungumza jana jijini na waandishi wa habari kwa niaba ya wanachama wenzake waliohama, Pamba alidai uongozi wa Kanda ya Pwani haukufuata Katiba ya chama ulipotangaza kuwavua uongozi bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.

Alidai hatua hiyo imelenga kumpendelea mmoja wa watia nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Ubungo ambaye hata hivyo, hakumtaja.

“Mimi Renatus Pamba, nilitia nia kugombea ubunge wa Ubungo na baada ya kuonyesha nia hiyo, figisu zikaanza za kuvunjwa uongozi niliokuwa ninauongoza mimi Kamati ya Utendaji ya Jimbo," alidai.

Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Jimbo hilo, Alex Sebastian, alidai kuwa kitendo cha kuvunjwa kwa uongozi wa jimbo hilo saa saba za usiku na uchaguzi wa viongozi hao kufanyika asubuhi, ni ishara ya wazi ya kutokufutwa kwa misingi ya kidemokrasia ya chama hicho.

Alisema hatua hiyo ilichukuliwa kwa malengo maalumu ya mtia nia mmoja wapo wa ubunge katika jimbo hilo kuweka safu yake.

“Tunatambua kuwa uongozi wa kanda unaweza kuwa na mamlaka zote za kuvunja uongozi, lakini ni lazima kufuata katiba," alidai Sebastian.

“Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani na Katibu wa Kanda, Ndugu Hemed Ally pengine hawaifahamu vizuri Katiba," aliongeza.

Baadhi ya watia nia katika Jimbo la Ubungo walioomba ridhaa ya chama hicho kuwania ubunge ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wake, Saed Kubenea na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.

Habari Kubwa