Vigogo wadaiwa kufadhili mtandao wa ujangili

15Jun 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Vigogo wadaiwa kufadhili mtandao wa ujangili

MKURUGENZI wa Kuzuia Ujangili nchini, Robert Mande, amesema baadhi ya viongozi wa serikali, taasisi za umma na binafsi wanafadhili mtandao wa ujangili wa wanyamapori.

Mande, alikuwa kizungumza hivi karibuni na waandishi wa habari 20 wa Tanzania na Thailand walioko kwenye programu ya kuandika habari za kupinga ujangili, iliyowezeshwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania, kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

 

Alisema biashara ya ujangili ina makosa mengi na hivi karibuni wamebaini makosa yanayofanywa na wataalamu walioko serikalini, mashirika ya umma, mashirika binafsi ambao wamepewa dhamana ya kusimamia rasilimali.

 

Alisema watu hao huwezesha ujangili kuendelea na kuharibu ushahidi au kesi za ujangili nchini, jambo ambalo lilifanya kazi hiyo kuwa ngumu, lakini kadiri wanavyokamatwa na kufikishwa mahakamani inasaidia.

 

"Ni biashara ambayo ilileta watu wenye uchu wa kutajirika haraka, ni biashara inayounganisha makosa mengi kama rushwa, utakatishaji wa fedha na ujangili," alifafanua.

 

"Mtaalamu akijiingiza kwenye rushwa ya kughushi inaitwa "white color crime' tumegundua ndilo tatizo kubwa kuliko lote, ushiriki wa wataalamu maeneo mbalimbali ndiyo unasababisha uhalifu kuendelea na kuwa mgumu kupambana nao," alisema.

 

Alisema ni rahisi kwa mtu mwenye nafasi kushawishiwa kushiriki kwenye uhalifu bila kujulikana kutokana na nafasi yake.

 

"Kupambana na mhalifu ambaye humjui na ana nafasi kwenye udhibiti wa sheria ni ngumu sana, tunashirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwenye kikosi chetu ili tuweze kupambana na watu wote kuanzia ngazi ya chini hadi juu," alisema.

 

Mande alisema muunganiko wa vyombo hivyo umeleta mafanikio makubwa na ndiyo maana kesi ya ‘malkia wa tembo’ ilihukumiwa na alifungwa miaka 17 na kulipa faini ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 20.

 

"Kuanzia mwaka 2016 hadi sasa ujangili wa tembo umeshuka sana, haya ni matunda ya ushirikiano baina ya vyombo vyote vya serikali na sekta binafsi," alibainisha.

 

Alisema ujangili ulikuwa tishio miaka ya 2000 hadi 2014, asilimia 60 ya tembo walitoweka na ndipo serikali ilianzisha mpango wa kitaifa wa kupambana na ujangili.

Alisema lengo ni kukabiliana na ujangili, biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya misitu na ilifanyika operesheni tokomeza kuonyesha ukubwa wa tatizo.

Mande ambaye ni Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kuzuia Ujangili nchini, alisema biashara hiyo ilishamiri kutokana na bei kuwa kubwa nchi za Asia kwa kuwa kilo moja iliuzwa  Dola 500 ikiwa Tanzania na ikiwa China ni Dola 2,000.

Habari Kubwa