Vigogo waibua upekee wa Lowassa

12Feb 2024
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Vigogo waibua upekee wa Lowassa

NCHI inaomboleza kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (70), huku wanasiasa wakiibua mambo mbalimbali yanayoonesha upekee wake kisiasa na kiuongozi.

Lowassa aliweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa wadhifa huo kujiuzulu mbele ya Bunge, kuhamia upinzani na kugombea urais huku akiwa ni mwanasiasa mwenye nguvu na aliyetikisa katika kila nyadhifa alizoshika.

Jana viongozi na wananchi walimiminika nyumbani kwa Lowassa, Masaki jijini Dar es Salaam kuifariji familia huku wakimwelezea kama kiongozi shupavu, aliyesimamia alichokiamini na mwenye kufanya uamuzi mgumu pasi na kuogopa huku akitanguliza mbele maslahi ya nchi.

Lowassa anatajwa kuwa kiongozi aliyekuwa na nguvu ya ushawishi ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hata alipokatwa kugombea nafasi ya urais mwaka 2015, alihamia CHADEMA na baada ya matokeo ya urais kutangazwa, wafuasi wake walitaka kuingia mtaani lakini aliwatuliza na kusema kuwa hataki urais wa utokanao na kumwaga damu za watu.

Katika mitandao ya kijamii zimesambazwa picha za 'mafuriko yake' ya watu wakati akirudisha fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya CHADEMA kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Posta, jijini Dar es Salaam pamoja na mikutano ya hadhara katika majiji ya Mbeya, Dar es Salaam, Arusha iliyochagizwa na kaulimbiu ya "Mabadiliko Lowassa! Lowassa Mabadiliko!"

KUZIKWA JUMAMOSI

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza mazishi ya mwili wa Lowassa yatakayofanyika Februari 17, mwaka huu katika Kijiji cha Ngarash, wilayani Monduli, mkoani Arusha.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alibainisha hayo jana alipotoa salamu za pole kwa familia ya marehemu nyumbani kwa Lowassa, Masaki, jijini.

“Watanzania pamoja na wanafamilia tutaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuupeleka mwili kwenye nyumba ya milele," alisema Waziri Mkuu.

Alisema ratiba ya safari hiyo itaanzia kesho ambapo mwili wa marehemu utafanyiwa ibada fupi na kuagwa na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Viwanja vya Karimjee kuanzia saa 2:50 asubuhi mpaka saa saba mchana kisha utarudishwa Hospitali ya Jeshi Lugalo.

Alisema kuwa Jumatano mwili utatolewa nyumbani hadi Kanisa la KKKT Azania Front kwa ajili ya misa takatifu inayotarajiwa kuanza saa nne asubuhi hadi saa saba mchana na waombolezaji watakaokuwapo kanisani watapata nafasi ya kuaga mwili.

Alisema kuwa Alhamisi mwili utasafirishwa kwenda Arusha kwa kutumia ndege. Watatua Uwanja wa Ndege Arusha au Kilimanjaro (KIA). Maelekezo kuhusu hili yatatolewa baadaye na wanatarajiwa kufika Monduli saa nane mchana.

Alisema kuwa Ijumaa, wananchi wa Monduli wataaga mwili wa aliyekuwa mbunge wao (1990-2015).

Lowassa aliwahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), Waziri wa Ardhi na Makazi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umaskini), Waziri wa Maji na Mifugo na mwaka 2005 aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu.

FREEMAN MBOWE

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ametuma salamu za pole kwa familia na kueleza kuwa taifa litamkumbuka Lowassa kwa mambo mengi kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.

Mbowe alisema amepokea kwa mshtuko na majonzi taarifa za kifo cha Lowassa, amempoteza rafiki, ndugu na mshauri mzuri.

"Tanzania na dunia imepoteza kiongozi shujaa, mwenye mchango mkubwa katika kujenga amani, ushirikiano na ustawi wa jamii.

"Alikuwa kiongozi shupavu, mwanasiasa mahiri, mwanaharakati hodari na alikuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini mwetu," alisema Mbowe akimtaja Lowassa alikuwa mtu mwenye hekima, busara, ujasiri, uzalendo, huruma, upendo na msamaha kwa wote, mtu mwenye maono, mipango na mtekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

"Tutaendelea kuenzi kazi, mawazo na hekima alizotuachia Mheshimiwa Lowassa. Tutaendelea kumwombea na kumkumbuka kwa mema aliyotutendea,” alisema Mbowe.

JAJI WARIOBA

Viongozi waliofika nyumbani kwake jana ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, aliyesema taifa limepoteza kiongozi mwenye upendo, utu na aliyepinga kuoneana kwenye siasa.

Alisema alimfahamu Lowassa kama kiongozi mwenye msimamo na asiyekata tamaa, aliyeamini katika elimu na ajira kwa vijana na hata alipokuwa Waziri Mkuu, alianzisha shule za sekondari za kata ili kuboresha upatikanaji elimu na kuwezesha watoto wa kitanzania kuendelea na masomo.

Kwa mujibu wa Warioba, wakati wa uongozi wake, Lowassa alikuwa mfuatiliaji mzuri wa utekelezaji wa yale yaliyoazimiwa na serikali.

“Pamoja na matatizo, Lowassa hakutetereka, aliendelea kuwa kiongozi, alikuwa na maono na imani yake,” alisema.

NAZIRI KARAMAGI

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Naziri Karamagi, alisema Lowassa alikuwa akipinga kuoneana katika siasa, alisisitiza wanasiasa wawe kitu kimoja na kufuata utaratibu waliojiwekea, hali iliyosababisha mwaka 2015 wapinzani kupata viti vingi.

Alisema pia alibadilisha dhana ya kilimo kwanza kuwa elimu kwanza, akiamini kuwa bila elimu hakuna kilimo, hali iliyochangia kuwa na wakulima wasomi.

Alisema yeye ni mmoja wa watu walioshawishiwa na kiongozi huyo kuingia kwenye siasa mwaka 2003 na tangu wakati huo alikuwa naye bega kwa bega akimwongoza na kumpa ushauri.

"Ukianguka ataanguka na wewe, ukisimama atasimama na wewe, hivyo ndivyo alivyokuwa Lowassa na ndio maana watu wengi walikuwa wanampenda," alisema.

BALOZI ADADI

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania Zimbabwe na Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu alisema Lowassa alipenda maendeleo ya watu na hakupenda kuona wananchi wanaishi maisha ya shida.

Balozi Adadi ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), alitolea mfano kuwa alikwenda Misri kujenga hoja ili wananchi wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na mengineyo wapate maji yanayotoka Ziwa Victoria na alifanikiwa na sasa wananufaika.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, alisema anamkumbuka mwanasiasa huyo wa utu wake na wakati wa uongozi wake alitumikia wananchi kwa moyo mmoja. Alijifunza kwake uzalendo na kuipenda nchi kwanza.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Goodluck Ole-Medeye, alisema Lowassa alikuwa anapenda watu wote na hakukubali kuona yeye ameshiba ilhali mtu mwingine ana njaa, alikuwa kiongozi mnyenyekevu na asiyependa majungu.

"Alikuwa mbunifu na mwenye mawazo mapana, hata siku moja huwezi kumkuta akimteta mtu, alitaka ukienda kwake uende na mawazo au mapendekezo ya maendeleo," alisema.

ACT WAZALENDO

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT- Wazalendo, Juma Haji, alisema kuwa wakati wa uhai wake, Lowassa alikuwa kiongozi aliyetumikia nchi kwa moyo mkunjufu katika nafasi mbalimbali alizoshika.

Duni alisema chama chao kimetangaza bendera zake zitapepea nusu mlingoti kwa siku tano za maombolezo zilizotangazwa na Rais Samia.

RAIS KARUME

Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume alisema Lowassa alikuwa mchapakazi, mwenye uthubutu katika kufanya uamuzi na maisha yake ya siasa kwa ujumla.

Rais huyo mstaafu alisema taifa limepoteza mtu ambaye alikuwa shupavu katika siasa za Tanzania na "hodari sana".

Karume alisema akiwa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar waliendelea kushirikiana zaidi na Lowassa ambaye wakati huo alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.

"Tulipokuwa bungeni tunapitisha muswada kuruhusu mfumo wa vyama vingi, ninakumbuka wale wenzangu na mimi tulikuwa kundi moja tulikuwa tunaunga mkono muswada ule, kwa sababu tuliona ungepeleka nchi yetu mbele zaidi na Lowassa alikuwa mmoja wa ‘machampioni’ kwa demokrasia ya nchi yetu hii," alisema Karume.

Kuhusu kujiuzulu kwa Lowassa katika nafasi ya Waziri Mkuu, Karume alisema hilo ni jambo la kawaida kisiasa na kwa wanasiasa kama ajali ya kisiasa na kwamba yeye (Karume) halikumshtua.

PROF. TIBAIJUKA

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka aliandika katika ukurasa wake wa X; “Familia ya Lowassa poleni. Taifa twaomboleza kifo cha kjiongozi ‘STATESMAN’. Nilishuhudia ukiweka maslahi ya nchi mbele ya yako.

"Jina lilipokatwa nilikushauri ubaki CCM kimfumo uwezekano kutangazwa mshindi ukitokea upinzani HAUPO, ukanijibu 'NAJUA ila hutaki Manyanyaso kuendelea'. R.I.P."

SWAHIBA MGEJA

Khamisi Mgeja, aliyekuwa Mwenyekiti CCM Mkoa wa Shinyanga na kuamua kuacha wadhifa wake akimfuata swahiba wake wakati huo Lowassa anahamia CHADEMA, alisema jana kuwa kiongozi huyo alikuwa mtu mwenye uthubutu kiutendaji.

“Haikujalisha kwa kipindi hicho tulikuwa wengi tulioamua kujitoa mwanga bila kujali maslahi ya nafasi zetu kwa kauli moja kwani tuliamini kuwa kiongozi huyo alikuwa na uwezo mkubwa wa kiutendaji na pia alikuwa na uthubutu katika kuwatetea wananchi pamoja na taifa kwa ujumla," alisema Mgeja.

Agosti 13, 2015 Mgeja alitangaza kujiuzulu nafasi zake ndani ya CCM na kuhamia CHADEMA kwa kauli waliyoitumia kuwa "CCM si baba yangu, siyo mama yangu, Watanzania wanahitaji mabadiliko".

“Hata alipokuwa CHADEMA hakutaka vurugu wala kuona damu za Watanzania zinamwagika kisa yeye, hivyo alizuia maandamano yaliyotakiwa kufanya na vijana licha ya kujua kuwa alikuwa ameshinda uchaguzi huo na kwa hilo tu kila mwanasiasa anayewatetea wananchi hawezi kuacha kuenzi maisha ya Lowassa," alisisitiza Mgeja.

SWAHIBA MSINDAI

Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Mgana Msindai, alisema taifa limempoteza kiongozi mahiri aliyekuwa mtawala wa kutukuka, asiyeogopa na alifanya uamuzi wa mambo ya maendeleo na kuyasimamia hadi yakaleta matokeo chanya.

Msindai alisema Lowassa atakumbukwa kwa mengi aliyoyafanya wakati wa uhai wake, lakini kubwa zaidi ni kuanzisha shule za sekondari za kata ambazo kwa sasa zinatawala na zimeanza kufaulisha vizuri.

Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye alikuwa swahiba wa Lowassa, Peter Serukamba, alisema amepokea kwa masikitiko kifo cha Lowassa na taifa limepoteza mmoja wa wazalendo wake.

HARRISON MWAKYEMBE

Waziri mstaafu katika wizara mbalimbali, Dk. Harison Mwakyembe alisema amepokea taarifa ya kifo cha Lowassa kwa masikitiko makubwa kwa kuwa Watanzania akiwamo yeye (Dk.Mwakyembe) walikuwa wanahitaji mchango wake wa mawazo.

"Hili halina ubishi kwamba Lowassa alikuwa hazina kubwa ya mawazo na ushauri chanya katika ujenzi wa taifa letu.

"Nitumie nafasi hii kuitakia familia ya marehemu na Watanzania wote wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezi," alisema.

ALBERT CHALAMILA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema Lowassa aliwafundisha namna kiongozi anapaswa kuwa na uvumilivu wa kisiasa katika uongozi.

Alisema kiongozi huyo alikuwa ni mwalimu na daraja la usuluhishi katika siasa na mara zote alionesha kuwa siasa si uhasama kwa kuwa nia ni moja - kutumikia wananchi.

PAUL MAKONDA

Jana Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda, alitangaza kusitisha ziara yake ya mikoa 19 ambayo ilibaki ya Mtwara na Lindi ili kuomboleza kifo cha Lowassa.

"Kwa mashauriano na hekimu kubwa iliyotuongoza tumeona ni vyema kuahirisha ziara ili tuungane na Watanzania wote katika kipindi hiki cha maombolezo na sisi CCM ambacho amekitumikia tangu akiwa kijana ameshika nafasi nyingi, tuwaombe wananchi katika mikoa iliyobaki ya Mtwara na Lindi ziara yetu tutaipanga tena," alisema Makonda.

Juzi alasiri, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango alitangaza kifo cha Lowassa na kubainisha kuwa Rais Samia ametangaza siku tano za maombolezo kitaifa kuanzia juzi.

*Imeandaliwa na Jenipher Gilla, Elizabeth Zaya, Beatrice Shayo (DAR), Thobias Mwanakatwe (SINGIDA) na Vitus Audax (MWANZA)