Vigogo watatu wa hal. watumbuliwa

20Dec 2016
Gideon Mwakanosya
SONGEA
Nipashe
Vigogo watatu wa hal. watumbuliwa

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya Songea Vijijini mkoani Ruvuma, limewasimamisha kazi vigogo watatu wa halmashauri hiyo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka yao kwa kubadilisha matumizi ya fedha bila kufuata taratibu.

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya Songea Vijijini mkoani Ruvuma.

Kati ya waliosimamishwa yumo Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Mwajuma Sekelela.

Wengine ni Ofisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Wenisalia Swai na Ofisa Ugavi na Manunuzi, Amina Njogela.

Akitoa tamko la kuwasimamisha kazi vigogo hao juzi kwenye kikao maalum cha baraza hilo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Rajabu Mtiula, alisema Baraza limefikia uamuzi huo baada ya kutambua kuwa watumishi hao ambao ni wakuu wa idara, walikiuka taratibu za matumizi ya fedha ndani ya idara zao.

Mtiula alisema walifanya hivyo bila kushirikisha Kamati ya Mipango na Fedha, jambo alilosema ni kinyume cha sheria.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Simon Bulenganija, alifafanua kuwa watumishi hao walibadilisha matumizi ya fedha ya miradi mingine na kumlipa mkandarasi aliyejenga jengo la makao makuu la halmashauri hiyo lililopo katika kijiji cha nje kidogo ya mji mdogo wa Peramiho.

Bulenganija alisema Swai ambaye kipindi hicho alikaimu Ukurugenzi wa halmashauri hiyo na Sekelela (Mweka Hazina), wana tuhuma zinazofanana ya kuidhinisha fedha za ukarabati wa Kituo cha Afya cha Mhukuru na fedha za mradi wa umwagiliaji wa bonde la Nakauga.

Pia wanatuhumiwa kumlipa mkandarasi bila Kamati ya Fedha na Mipango na kuhusishwa. Alisema kuwa kwa mtumishi Njogela (Ofisa Ugavi na Manunuzi), anatuhumiwa kuchelewesha zabuni za mradi wa umwagiliaji wa bonde la Nakauga bila sababu za msingi.

Hata hivyo, alisema baadaye iligundulika kuwa mradi huo fedha zake zimetolewa kwa kubadilisha matumizi kwenda kumlipa mkandarasi.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa moja ya sababu zilizokuwa akizitilia shaka kuipokea ofisi kwa kwa haraka kwa makabidhiano tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli, ni pamoja na taratibu za miradi hiyo ambayo ilikuwa haijawa wazi matumizi yake.

Alisema atawaandikia barua watumishi hao kwa mujibu wa kanuni pamoja na kuunda kamati itakayofanya uchunguzi wa jambo hilo kisha kutoa majibu sahihi ya fedha zinazodaiwa kubadilishwa matumizi yake.

Habari Kubwa