Vigogo wengine waachiwa msamaha wa Rais

09Oct 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Vigogo wengine waachiwa msamaha wa Rais

MKURUGENZI Mkuu wa Benki M Tanzania, Sanjeev Kumar (63), ameachiwa huru baada ya kutakiwa kulipa fidia ya zaidi ya Sh bilioni 6.03 kutokana na kukiri makosa yake na jana, alilipa Dola za Kimarekani 300,000 sawa na Sh. milioni 690.

Mahakama imemtaka Kumar kulipa fidia hiyo ndani ya miezi 24 na endapo atakiuka makubaliano hayo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) atamchukulia hatua.

Hukumu hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Uamuzi huo umekuja baada ya upande wa mashtaka kumfutia mashtaka ya uhujumu uchumi na kumsomea mashtaka mawili ya kuisababishia serikali hasara.

Baada ya kusomewa mashtaka yake, mshtakiwa alikiri kufanya makosa hayo.

Akisomewa hukumu yake na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, alisema katika mashtaka hayo mawili mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh. milioni moja kwa kila kosa.

Alisema mshtakiwa atatakiwa kulipa fidia ya Sh. 6, 039,103,579 na atailipa kwa miezi 24, kwa kila mwezi kulipa kiasi cha Sh. milioni 222.8.

Hakimu Shaidi alisema hati ya kusafiria ya mshtakiwa huyo itabaki katika Ofisi za DPP na safari zake zote zitafuatiliwa na ofisi hiyo.

Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Jaquline Nyantori, alidai kuwa hawana rekodi ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa hivyo, aliomba mahakama itoe adhabu kulingana na makubaliano ili iwe fundisho kwake na wengine.

Wakili Nyantori alidai kuwa wameingia makubaliano na mshtakiwa huyo baada ya kukiri kosa la kuisababishia serikali hasara wameamua kuondoa mashtaka ya kughushi, kutakatisha fedha, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Baada ya kusoma makubaliano hayo, Hakimu Shaidi alimuapisha mshtakiwa na kumuuliza kama alisaini kwa hiari yake na kudai alifanya hivyo kwa hiari yake.

Akisoma mashtaka mapya, Wakili Nyantoru alidai katika shtaka la kwanza, Januari 20, 2016 mshtakiwa huyo akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki M Tanzania kwa vitendo vyake alivyovifanya aliisababishia serikali kupata hasara ya Sh. 6,039,103,579.

Alidai katika shtaka la pili, mshtakiwa huyo anadaiwa Januari 20, 2016 akiwa katika Jiji la Dar es Salaam kwa njia ya ulaghai ndani ya Benki M Tanzania akijua ni udanganyifu alijipatia Dola za Marekani 287,000.

Katika hatua nyingine, mfanyabiashara David Mudi na wenzake wanne, wamehukumiwa kulipa fidia ya Sh. milioni 40 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na nyara za serikali bila kibali.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mohamed Salum Mohamed, Mustapha Bakari, Salum Wakili na Shabani Haji.

Washtakiwa hao walipewa adhabu hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Janet Mtega.

Washtakiwa hao walipewa adhabu ya kifungo cha nje kwa sharti na kutofanya kosa hilo tena na washirikiane na serikali kutoa taarifa za watu wengine wanaojihusisha na makosa kama hayo.

Hakimu aliwaeleza washtakiwa hao kuwa, watalipa fidia hiyo ya Sh. milioni 40 kwa utaratibu uliooneshwa katika hati ya makubaliano.

Washtakiwa hao ni miongoni mwa waliomwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri na kuomba msamaha.

Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Novemba mosi hadi 16 mwaka 2015, Zanzibar na Dar es Salaam, walijihusisha na usafirishaji wa kobe 201 wenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 30 bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyamapori.