Vijana 500 Chadema kuwania udiwani, ubunge

30May 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Vijana 500 Chadema kuwania udiwani, ubunge

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limesema wapo vijana zaidi ya 500 waliojitokeza kuwania nafasi za udiwani na ubunge kutoka katika chama hicho katika kata na majimbo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika gumzo la Nipashe linalofanyika katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa twita, Mwenyekiti wa Baraza hilo, John Pambalu, alisema kujitokeza kwa vijana hao ni ishara ya hamasa iliyopo katika taifa kwa sasa katika kupigania maendeleo ya nchi yao.

“Vijana katika taifa lolote ndio wachochezi wakubwa wa maendeleo ya nchi, sisi kama vijana tunapata faraja kuona idadi hiyo kubwa ikijitokeza kuwania nafasi hizo ni ishara ya mafanikio kwetu,” alisema Pambalu.

Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, unatarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu huku kila chama kikipanga mikakati yake na kuandaa wagombea katika uchaguzi huo, wakati chama hicho kikuu cha upinzani nchini kikifunga hatua ya watu kujitokeza kutia nia kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, Chama cha ACT- Wazalendo, kilifungua hatua hiyo mwezi uliopita.

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT -Wazalendo, Ado Shaibu, aliagiza tangu Aprili 30, mwaka huu, makatibu wa kata na majimbo wa chama hicho kuandaa madaftari ya kuorodhesha watia nia katika maeneo yao ili kupata idadi ya watia nia katika chama hicho.

Aliwataka watia nia hao kuzingatia maadili, utu na utamaduni wa chama hicho wanapotangaza nia zao hizo na kuomba msaada wa kuunganishwa na vyombo vya habari ili kujitangaza inapobidi katika idara ya uenezi ya chama hicho, mpaka sasa wanachama kadhaa wa chama hicho wakiwamo vijana wamekwisha jitokeza hadharani kutangaza nia.

Habari Kubwa