Vijana wa kike watakiwa kugombea nafasi za kisiasa

20Nov 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Saalam
Nipashe Jumapili
Vijana wa kike watakiwa kugombea nafasi za kisiasa

MKURUGENZI Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, amewataka vijana wa kike kujitokeza kuwania nafasi za kisiasa ili washiriki mchakato wa kujenga taifa kwa kuwa kwenye siasa ndiko maamuzi mengi na mazito hufanyika.

MKURUGENZI Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi,

Akizungumza wakati wa mafunzo ya siku tatu ya uongozi wa kifemina kwa viongozi wanawake, kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Saalam, Nyanzobe Mwakaiya, alisema vijana wengi hawana kadi za vyama na hawagombei nafasi husika.

“Ni wangapi miongoni mwenu wana kadi ya chama cha siasa? naona ni wachache sana sasa utawezaje kufika ngazi ya maamuzi kama hata kadi ya chama huna, ni lazima tuwe na kadi na tushiriki shughuli za vyema kwenye maeneo yetu na zaidi tugombee nafasi bila kuogopa.”alisema.

“Chukueni nafasi za uongozi, uongozi sio misuli . Siasa ni kila kitu, tukiwa na viongozi wengi kwenye siasa itasaidia kubadili sheria, sera zetu. Bungeni vijana ni wachache sana na wasichana ndio wachache zaidi, tushuke nafasi tulete mabadiliko,”alifafanua.

Liundi alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuimarisha uwezo wa uchambuzi wa kifeminia na kuongeza uwajibikaji kwenye maeneo yao.

“Mafunzo haya ni muhimu sana kwenu yana malengo mahususi ya kuongeza uwezo wa kutofautisha kati ya uchambuzi wa kijinsia na wa kifemina, kuongeza uelewa wa dhana za uongozi wa kijinsia na kifemina, kuongeza uwezo wa kutumia kanuni za kifemina katika shughuli zenu na kutengeneza mpango kazi na kubadilishana uzoefu,”alisema.

Alisema uongozi thabiti na imara ni fursa ya kipekee kwa vijana wadogo, uongozi wa kifeminia ni kama unavyoona msitu wenye kila kitu ndani tukiangalia hatusemi huu ni msitu bali tunauchambua kwa kwa kina kwamba ndani yake kuna nini.

“Kwenye uongozi wa kifeminia tunaangalia changamoto kama fursa na namna ya kusonga mbele. Sensa ya mwaka huu imeonyesha vijana ni zaidi ya asilimia 60, wanawake ni asilimia 50 lakni tukiangalia kwenye uongozi wanawake ni wachache sana na hiyo inakwenda hadi ngazi ya shule,”alisema.

Liundi alisema takwimu za dunia kiuongozi marais wanawake ni 21, huku viongozi wengine na asilimia zao kwenye mabano ni Spika (29), Naibu Spika (28.3) na wabunge wote (25.5), kwa Afrika Mashariki Rwanda inaongoza kwa kuwa na wabunge wanawake (61.3) huku Tanzania ikiwa ni (36.7).

Aidha, alisema Tanzania imebahatika kuwa na wanawake wanaoongoza mihimili miwili ya nchi ambayo ni Rais Samia Suluhu Hassan na Spika Dk. Tulia Ackson huku hali sio nzuri kwneye serikali za mitaa ambazo madiwani ni (29.4) kati yao wa kuchaguliwa ni asilimia saba.

Pia kwenye vitongoji na vijiji na asilimia zao kwenye mabano viongozi wanawake kwenye vijiji  (2.1), vitongoji (6.7) na kwamba kwa ujumla serikali za mitaa ni chini ya asilimia 10.

Akifungua mafunzo hayo, Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Nyanzobe alisema kuna changamoto nyingi za kuwa kiongozi lakini kuna fursa nyingi ambazo zina faida kubwa huku akiwataka vijana hao kutoogopa kuonyesha uwezo wao.

Alizitaja fursa zilizopo ni nafasi ya kuzungumza kwenye vikao, mkutano na semina mbalimbali, kujengwa kisaikolojia kuwa na nguvu ya kuwasemea na kuwapigania wengine, kuongeza mtandao na kutembea ndani na nje ya nchi.

Habari Kubwa