Vijana wa Somalia kusomea uvuvi Bagamoyo

29Feb 2016
Frank Monyo
Nipashe
Vijana wa Somalia kusomea uvuvi Bagamoyo

SHIRIKA la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kupitia Wizara ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, wataendesha mafunzo ya uvuvi kwa vijana 15 kutoka nchini Somalia

Wavuvi wakivua samaki

Mafunzo hayo ya majaribio yanatarajiwa kuanza Mei, mwaka huu, katika chuo cha Maendeleo ya Uvuvi Mbegani, Bagamoyo, yana lengo la kuongeza ajira na kupunguza uvuvi haramu na uharamia katika Bahari ya Hindi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki na waandishi wa habari pamoja na ujumbe wa Serikali ya Somalia, Mkurugenzi Mwakilishi wa JICA, Toshio Nagase, alisema mafunzo hayo yanalenga kujenga amani ya nchi hiyo na kuondokana na uvuvi haramu na kuongeza wigo na fursa ya ajira kwa vijana.

Alisema baada ya mafunzo hayo yatakayo dumu kwa mwezi mmoja katika chuo cha Mbegani, wahitimu hao watawafundisha vijana wa Somalia juu ya uvuvi.

Alisema wamechagua Mbegani kwa sababu ni maarufu katika nchini za Afrika za Mashariki kwa kutoa mafunzo bora katika sekta ya uvuvi.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Wizara ya Mipango na Maendeleo ya Somalia, Mohamed Farah, alisema baada ya vita ya muda mrefu nchini humo, serikali imeanzisha mpango wa kuongeza ajira kwa vijana.

Alisema nchini Somalia, asilimia 75 ya watu ni vijana na kati ya vijana hao wana umri kati ya miaka 14- 42 hawana ajira.
Naye Mshauri Mwandamizi wa Wizara ya Uvuvi na Rasilimali za Bahari wa Somalia, Omar Abdulle Hayle, alisema watahakikisha vijana wanapata vifaa vya kisasa vya uvuvi na kujishughulisha katika sekta hiyo na kuachana na shughuli haramu.

Alisema sheria ya uvuvi ya Somalia inalenga kutoa fursa kwa vijana kujiingiza katika sekta hiyo na kuacha kujiingiza katika makundi ya kigaidi ili kujipatia ajira na kuongeza usalama wa chakula.

Habari Kubwa