Vijana waaswa kuchangamkia fursa

26Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Vijana waaswa kuchangamkia fursa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kwa kuanzisha vijiwe vya kiuchumi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na vijana walionufaika kupitia kituo cha maendelo ya vijana, Sasanda.

Kauli hiyo ameitoa wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo na miradi ya vijana iliyopo katika Kituo cha Maendeleo ya Vijana, Sasanda kilichopo Kata ya Nyimbili, Mkoani Songwe.

Mhe. Mhagama ameeleza kuwa, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeendelea kutimiza azima yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo vijana watumie fursa hiyo kujifunza mambo muhimu na kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawafanya wabadilishe vijiwe wanavyokaa kuwa vya kiuchumi.

“Tunataka kuona vijana watakapo jifunza kilimo bora, ufugaji wa ng’ombe au nyuki wataweza kuboresha thamani mazao na bidhaa kwa kuanzisha viwanda vidogo ndani ya Mkoa wa Songwe, mkakati wetu katika kituo hiki ni kutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana kuongeza thamani ya mazao na bidhaa watakazozalisha ambazo zitakuwa ni kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo yao” amesema Mhagama

Ameongeza kuwa, Takribani vijana 500 kwenye kituo hicho wamejifunza stadi za maisha, ufundi na elimu mbalimbali zinazotolewa kwenye kituo ambazo zitawawezesha kujipatia kipato. 

Habari Kubwa