Vijana wanaoishi mazingira hatarishi wanufaika na ‘Dream’

14May 2017
Nebart Msokwa
Nipashe Jumapili
Vijana wanaoishi mazingira hatarishi wanufaika na ‘Dream’

ZAIDI ya vijana 970 wanaoishi kwenye mazingira hatarishi jijini Mbeya, wamenufaika na mradi wa kuwawezesha mabinti walio kwenye umri wa kuvunja ungo na wanawake wanaoishi katika mazingira hatarishi unaotekelezwa na Kikundi cha Huduma majumbani mkoani Mbeya (Kihumbe).

Meneja wa Kihumbe, Ptolemy Samwel.

Akizungumza na wandishi wa habari jana, Meneja wa Kihumbe, Ptolemy Samwel, alisema vijana hao wamewezeshwa masuala ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha ili ziwasaidie kuinua kipato.

Aidha, alisema vijana hao wamewezeshwa kujiunga na vikundi vya ujasiriamali 50 ndani ya kata zote 36 za Jiji la Mbeya ili waweze kujiendeleza na kukopesheka kirahisi na taasisi za kifedha na kuendeleza shughuli zao.

Alisema wengi wa vijana hao walikuwa wanaishi katika mazingira hatarishi ambayo yangewasababishia kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi pamoja na mimba zisizotarajiwa hasa kwa watoto wa kike kutokana na biashara ya ngono.

“Vijana hawa walikuwa wanaishi kwenye mazingira hatarishi, baadhi ya mabinti walikuwa wanafanya biashara ya ngono ambayo ingewasababisha kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi na mimba zisizotarajiwa,” alisema Samwel.

Mratibu wa mradi wa Dream, Anna Mcharo, alisema mradi huo ulianza mwezi Mei, mwaka jana na vijana hao walikuwa wanapatikana kwa kujaza madodoso maalumu na waliogundulika kuwa na sifa walichukuliwa.

Alisema mradi ulikuwa unawalenga zaidi wasichana na wanawake, lakini waliamua kuwaingiza wanaume ambao wengi wao ni wenza wa mabinti kwa ajili ya kutambua kinachofanyika na kuepuka kuibuka kwa unyanyasaji wa kijinsia.

Mchalo alisema vijana hao pia wamefundishwa njia mbalimbali za kuepuka unyanyasaji wa kijinsia, mbinu mbalimbali za uzazi wa mpango, njia za kuepuka maambukizi ya Ukimwi, na madhara ya mimba za utotoni.

Alisema lengo la mradi huo ni kuwafikia vijana 700 ndani ya Jiji la Mbeya kufikia mwezi Mei mwaka 2018, lakini mpaka sasa umewafikia vijana 976 kati yao wasichana ni 688.

“Mradi huu unakusudia kuwafikia vijana 7,000 na mpaka sasa tumewafikia hao 976 ambao wasichana wapo kwenye vikundi 32 vya ujasiriamali na wanaume wapo kwenye vikundi 18 hivyo kufanya vikundi kuwa 50,” alisema Mcharo.

Mmoja wa wasichana walionufaika na mradi huo, Upendo Anyambilile, alisema kabla hajaingia kwenye mradi huo alikuwa anafanya biashara ya ngono wakati akiwa na umri mdogo kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu.

Alisema katika biashara hiyo, alipata mimba isiyotarajiwa na kujifungua, lakini mwanaume aliyempa ujauzito huo aliukataa na kumtelekeza jijini Dar es Salaam mpaka aliposafirishwa na wasamaria wema kurudi Mbeya.