Vijana watahadharisha ndoa za utotoni

07Feb 2016
Efracia Massawe
Nipashe Jumapili
Vijana watahadharisha ndoa za utotoni

MUUNGANO wa vijana nchini unaojulikana kama Youth For Change, umeitaka serikali kuchukua maamuzi magumu ya kutunga sheria itakayosimaia na kupinga vitendo vyote vya kikatili dhidi ya mtoto wa kike hususani ndoa za utotoni na ukeketaji.

Picha ya Maktaba.

Vijana hao katika nyakati tofauti walisema hawaoni sababu ya serikali kushindwa kuweka sheria itakayowadhibiti watu wanaofanya vitendo hivyo katika jamii, hasa kwa kukatisha ndoto za watoto wa kike ambao ni viongozi wa taifa la sasa na lijalo. Waliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa kongamano la kupinga ndoa za utotoni na ukeketaji, lililoandaliwa na Shirika la Plan International Tanzania (Plan) kwa kushirikiana na Youth For Change na kuhudhuriwa na wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari. Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Jangwani, Betha Samwel, aliishauri serikali kutafuta njia ya kutokomeza vitendo hivyo vya kikatili katika jamii, na ione umuhimu wa kuthamini mchango wa watoto wa kike. “Wasichana wenzangu tuepuke vishawishi vinavyoweza kutuletea madhara ya ndoa za utotoni na ukeketaji, ni lazima tushikamane kwa pamoja tujitambue ili tufike malengo yetu ya baadaye,” alisema Betha. Mwanafunzi mwingine wa shule ya sekondari Kibasila Dar es Salaam, Nibson Nicsoni, aliwataka vijana kupaza sauti zao kupinga ukeketaji na ndoa za utotoni zinazoendelea kuwadhalilisha watoto wa kike kila siku nchini. Naye Mwanachama wa Youth For change, Upendo Bisai, alisema serikali bado ina kigugumizi katika suala la kutokomeza ndoa za utotoni na ukeketaji, hali ambayo imechangia kushamiri kwa matukio mengi dhidi ya watoto wa kike ndani na nje ya Dar es Salaam. “Dhamira yetu ni kuona ukeketaji unatokomezwa kabisa na sio kupunguzwa, katika historia za nchi zilizoendelea hakuna tafiti zinazoonyesha ukeketaji au ndoa za utotoni zina manufaa badala yake zinaharibu utu wa mtoto wa kike na mwanamke kwa ujumla,” alisema. Mwanachama mwingine Aristariki Joseph, alihoji kwanini serikali haina takwimu za matukio ya ndoa za utotoni na ukeketaji za kila mwaka ambazo ingeziweka wazi ili kuwapa mwongozo wadau wa afya ili waweze kuvalia njuga tatizo hilo. Akijibu kauli hizo kutoka kwa wanafunzi, Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara ya Sheria, Rose Minja, alisema serikali bado ina takwimu za mwaka 2010 ambazo zinabainisha kuwa asilimia 15 ya wanawake nchini wamekeketwa bila ridhaa yao. Alisema kupitia takwimu hizo, serikali bado itaendela kushirikiana na sekta binafsi, zikiwamo taasisi mbalimbali katika kupinga vitendo vya kikatili dhidi ya watoto wa kike hususani ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji. Pamoja na hilo, aliutaja mkoa wa Singida kuwa ndio unaoongoza kwa vitendo vya ukeketaji kwa watoto wadogo wa kike kulinganisha na mikoa mingine.

Habari Kubwa