Vijana watakiwa kuwa wabunifu

25Sep 2021
Halfani Chusi
Dar es Salaam
Nipashe
Vijana watakiwa kuwa wabunifu

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Ajira, Vijana, Kazi na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Muhagama, amewataka vijana kutokubweteka mahala pakazi na badala yake amewataka kuchapa kazi kwa bidii na kwa ubunifu.

Muhagama ameyasema hayo Jijini Dar Es Salaam,  wakati wa hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa hiari wa hali bora baina ya menejimenti ya makampuni ya Oryx na chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (Tuico).  

"Mimi binafsi kama Waziri mwenye dhamana ya kazi na ajira huwa nafarijika sana pale ninapo ona waajiri wanawajali wafanyakazi wao kwa kuchukua hatua stahiki kama hii ya leo, hiki ni kielelezo tosha kabisa kwamba Kampuni ya Oryx,  inania njema na wafanyakazi wake na hili ni jambo la kupongeza" amesema Mhagama

Katika hatua nyingine Waziri huyo aligusia baadhi ya vipengele vilivyopo katika mkataba huo nakusifu vipengele kwa kile alichosema kuwa mkataba huo umeweka maslahi ya mfanyakazi  mbele.

"Nimeona Kuna kipengele cha kuwalipia ada watoto wa wafanyakazi hongereni sana ni jambo zuri na nimeambiwa suala hili ni kwa wafanyakazi wote " alisifia

 Kwa upande wake Katibu Mkuu tuico, Boniface Mkakatisi,  aliwataka vijana wasibweteke wawe na ari ya kufanya kazi kwa moyo mmoja ili kuongeza tija na ufanisi zaidi katika utendaji wao wa kazi.

Vilevile Mkurugenzi Mtendaji Kampuni ya Oil , Kalpeshi Metha,  alimpongeza Raisi Samia, kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuahidi kuwekeza zaidi ili kuongeza fursa ya vijana wengi kupata ajira.