Vijiji 11 vyapatiwa vyeti vya ardhi na hakimiliki za kimila

29Oct 2019
Daniel Sabuni
ARUSHA
Nipashe
Vijiji 11 vyapatiwa vyeti vya ardhi na hakimiliki za kimila

VIJIJI 11  vilivyopo Wilaya ya Longido, Mkoani, Arusha vimekabidhiwa vyeti vya ardhi za vijiji na vyeti vya hakimiliki za kimila za maeneo ya pamoja ya nyanda za malisho ili kuepuka migogoro miongoni mwao inayopelekea umaskini.

Mwenyekiti wa kijiji cha Eworendeke Esupat Laiser.

Vijiji hivyo ni Ilchang’ Itsangishu, Gilailumbwa, Loondowuo, Orkejuloongishuu, Armanie, Eworendeke, Matale, Amairowa, Karao, Sinonik na Kimwati.

Ngalaikiti Laiser akisoma risala kwa kwa niaba ya wanakijiji mbele ya mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido Toba Nguvila aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Frank Mwaisumbe, amesema vyeti na hati hizo zimekabidhiwa kwa vijiji ambavyo ni muungano wa Tarafa tatu za Kitumbeine, Longido na Engarenaibo.

Amesema mradi huo wa miaka mitano, unaoelekea ukingoni mwishoni mwa mwaka huu, umewezeshwa na Shirika la “Ujamaa Community Resource Team” na kutekelezwa na mradi wa maisha bora.

“Mradi huo unajumuisha Kata za Gilailumbwa, Meirugoi, Kimokouwa, Ketumbeine Engarenaibor na Kata ya Matale ambazo kwa pamoja wamefanikiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa lengo la kulinda nyanda za malisho naardhi kwa ujumla na kusimamia kwa undelevu.,”amesema Laiser.

Mwenyekiti wa kijiji cha Eworendeke Esupat Laiser akipokea cheti cha hati miliki ya kimila kwa maneo la nyanda za malisho kwenye hafla ya kukabidhi vyeti na hati miliki za kimila za vijiji kutoka kwa Katibu Tawala ya Longido, Toba Nguvila hivi karibuni, Vijiji 11 vimefaidika na zoezi hilo kwa uwezeshaji wa Mradi wa Maisha bora kutoka shirika la UCRT, Picha na Daniel Sabuni.

Amesema zoezi hilo limetekelezwa kwa njia shirikishi sambamba na kujenga uwezo wa wanavijiji juu ya usimamizi wa matumizi bora wa ardhi na utawala bora na hivyo kusaidia kuepusha migogoro mikubwa kama ilivyokuwa awali kabla UCRT.

“Tumekuwa na migogoro ya mipaka iliyodumu takribani miaka 30 na kushindwa kupata ufumbuzi kati ya kijiji cha Kitale B na Wosiwosi na kukwamisha juhudi za maendeleo katika mpango wa matumizi bora ya ardhi na kupelekea kukosa amani kufuatia kutunishiana misuli hali inayoweza kuhatarisha usalama  wa raia na mali zao.," amesema

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Ujamaa Community Resource Team, Makko Sinandeu amesema wakati wa utekelezaji wa mradi wa maisha bora wakina mama wa jamii za kimasai nafasi zao zimeonekana kwa kuwa wameshirikishwa kikamilifu kuanzia mwanzo wa zoezi hilo hadi mwisho.

Amesema shirika lake linaamini baada ya utekelezaji huo wanavijiji wataitumia ardhi kwa utaratibu na mpango maalum ili matumizi yasiingiliane na kusababisha migogoro ambayo ni hatari kwa usalama wa watu, ardhi na uchumi wa Taifa.

“Vyeti hivi vinaipa mamlaka Halmashauri za vijiji kusimamia ardhi kwa sheria no 5 ya Mwaka 1999 na wanachi wanakaa na kupanga matumizi sahihi ya ardhi.,”amesema  Sinandeu.

Wakinamama wa jamii ya kimasai wakitumbuiza siku ya kukabidhiwa vyeti vya hati miliki za kimila za ardhi ya nyanda za malisho sherehe zikizofanyika kwenye kijijji cha Gilailumbwa wilayani Longido.

Awali Mratibu wa Mradi wa Maisha Bora na Mratibu wa Programu ya miradi inayotekelezwa Longido, Jamboi Baramayegu amesema mradi huo umetekelezwa na mashirika matano ya Kimataifa ya (VSF-B, IDP, TriasTanzania,WFP na Enabel kwa kushirikiana na mashirika mengine tisa ya Kitanzania.

Amesema mradi wa Maisha Bora ni wa aina yake maana unajumuisha sekta nne muhimu kwa maisha ambazo ni ardhi na mifugo, (UCRT&HEIFER), Maji, (Oikos&LCDO), Biashara (PWC, MVIWATA, TCCIA, LCDO na Lishe (Childreach).

Baramayegu amesema UCRT ambayo imefadhiliwa na nchi ya Ubeligiji zaidi ya shilingi bilioni 20 ilitegemewa kutekeleza matokeo tarajiwa ya kuwezesha upatikanaji wa uhakika wa ardhi iliyotengwa kwaajili ya malisho namatumizi endelevu ya raslimali zinazopatikana kwenye nyanda za malisho.

Programu ya  miradi ya longido ilianza Mwaka 2015 hadi 2019 wakati Mradi wa Maisha bora umefadhiliwa na serikali ya Ubeligiji kwa zaidi ya bilioni 20, wakati Mradi wa Engishon, Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la “African Initiative” na umeanza kutekelezwa mwaka 2019 na utafikia tamati 2021.

Habari Kubwa