Vijiji 20 havina umeme Ludewa

19Jul 2021
Elizabeth John
Njombe
Nipashe
Vijiji 20 havina umeme Ludewa

MBUNGE wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe, Joseph Kamonga, amesema kukosekana umeme katika vijiji 20, kunamkosesha usingizi na kuahidi huduma hiyo inawafikia.

Alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Lubonde, na kuonyesha kusikitishwa kwake na ukosefu wa umeme katika vijiji hivyo kiasi cha kuonekana ni jambo la anasa ilhali ni huduma ya lazima.

“Wananchi wanahitaji umeme wa uhakika, mradi wa uzalishaji unaomilikiwa na Kampuni ya Madope Hydropower, watu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakipita pita wanajua sisi tayari tunao umeme, lakini bado hautoshelezi kwa sababu ni wa mgao,” alisema Kamonga.

“Najua mnahitaji umeme hii ni kutengenezewa ajali ya kisiasa si ndiyo jamani? Kwa sababu wananchi watakuchukia sana kwenye vijiji vyote 20 hili jambo hata mimi linaninyima usingizi, ninahangaika usiku na mchana kushirikiana na mheshimiwa diwani wenu kuhakikisha kwamba wananchi wa kata hizi wanapata umeme wa uhakika,” alisema Kamonga.

Awali, wananchi wa Kata ya Lubonde walimwomba mbunge huyo kuwaletea nishati ya umeme ya uhakika ili aweze kufanya shughuli za kimaendeleo.

“Tunakuomba mheshimwa mbunge na sisi tuletewe umeme mbona sehemu nyingine kuna umeme wa uhakika, tunashindwa kuwa na miradi ya kiuchumi kwa sababu hakuna umeme wa uhakika, huu wa Madope usiku unakuwepo mchana hakuna,” alisema Philiph Kitulile.

Naye Grace Ngailo alisema changamoto ya kukosekana umeme wa uhakika ni kubwa na tatizo hilo linakwenda hadi kwenye zahanati zao.

“Sehemu kama zahanati kukosa umeme wa uhakika hii si sawa tunakua kama tupo nchi nyingine, tunamuomba mbunge wetu akaendelee kulisemea wananchi tunahitaji umeme,” alisema Grace.