Vikao Mahakama ya Rufani vyaongezwa

12Apr 2017
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Vikao Mahakama ya Rufani vyaongezwa

MAHAKAMA ya Rufani, imeongeza vikao vya kusikiliza kesi kutoka 11 hadi 15 kwa mwaka, ili kupunguza mrundikano wa mashauri.

Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma.

Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma, alisema hayo baada ya mkutano wa majaji wa Mahakama ya Rufani, uliofanyika jijini hapa mwishoni mwa wiki.

Alitaja changamoto inayosababisha mrundikano huo ni upungufu wa bajeti ya mahakama.

Alisema ukaguzi huo ulikuwa ukisaidia kupunguza makosa mbalimbali katika mahakama za chini ambazo husababisha rufani zisizo za lazima.

Alisema hatua walizochukua kupunguza mrundikano huo ni kufanya ukaguzi wa majalada kila baada ya miezi mitatu na kuhakikisha kumbukumbu za mahakama zinakamilika tayari kusikiliza.

Hatua nyingine ni kukusanya na kuweka takwimu sahihi katika mfumo wa rejesta za maandishi na pia katika mfumo wa kukusanya takwimu kwa kidijitali.

"Tunaimarisha usikilizaji mashauri Dar es Salaam ili tuyapunguze ya muda mrefu na tutatuma pia njia ya kuelimisha mahakama za chini kuhusu makosa ya uendeshaji yanayochochea rufani zisizo za lazima," alisisitiza.

Mahakama hiyo imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la mrundikano wa mashauri, kutokana na wananchi wengi kukata rufani kuliko zamani.

Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma, alisema mwaka 2012 mashauri 924 yalisajiliwa na yaliyoamuliwa ni 585 hivyo mlundikano uliongezeka kwa mashauri 339.

Alisema mwaka 2013 mahakama ilisajili mashauri 870 na kuamuliwa 850, mrundikano uliongezeka hadi mashauri 20 na mwaka 2014 yalisajiliwa 991, yalioamuliwa 1007 hivyo ulipunguzwa kwa mashauri 16.

Aidha, mwaka 2015 walisajili mashauri 1222, yalioamuliwa 883 na mrundikano uliongezeka hadi mashauri 229 na mwaka 2016 walisajili 1449 na kuamua 1273 hivyo mrundikano uliongezeka hadi mashauri 176.

Alisema mwaka 2016 mashauri yenye umri kati ya miaka mitano hadi 10 yalikuwa 346 na ya zaidi ya miaka 10 yalikuwa 105.

Aidha, alisema mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kuwa na mashauri ya umri mkubwa kwa asilimia 76 nchini, pamoja na kasi ya kumaliza mashauri ya mkoa huo ilifikia asilimia 93 mwaka 2016.

Habari Kubwa