Maelfu ya wananchi wa mkoa huo na jirani walijitokeza kuaga miili hiyo, huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongoza waombolezaji.
Aidha, miili 69 ilizikwa yote na ndugu walijitokeza kupima vinasaba ili itakapotambulika kila kaburi litawekewa jina, lakini kwa jana ilizikwa na kupewa namba.
Wananchi 48 walijitokeza kutoa vinasaba kwa ajili ya utambuzi wa ndugu zao, na kwamba wapo ambao hawakuzikwa jana kwa kuwa ndugu waliomba kuzika wenyewe.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya taifa hadi wilaya, ikiwamo Wilaya ya Njombe ambako ndiko iliko Kampuni ya Chesco ambayo inamiliki gari lililolipuka na kuunguza idadi kubwa ya watu.
Mmoja wa ndugu wa marehemu, Omari Juma, alisema mtoto wa kaka yake alifariki na alikwenda Muhimbili kutambua katika majeruhi, lakini hakuona.
“Anaitwa Hassan Dachi hayumo katika majeruhi wala waliotambulika, lakini baada ya kupima vinasaba alitambulika na walikubali azikwe kwenye eneo hilo,” alisema.
Aliwataka Watanzania kujifunza kutokana na tukio hilo wanaposikia mshtuko wasikimbilie, ikiwamo serikali kutoa elimu ya mara kwa mara kwa kuwa wapo waliokufa ambao walikwenda kuangalia.
Alisema wazazi wamepata hasara kwa kuwa waliokufa wengi ni vijana na kwamba mtoto wake alikuwa mchezaji wa mpira.
Miili hiyo ilianza kuzikwa majira ya saa 11 jioni, viongozi wa dini mbalimbali waliweka udongo kwenye makaburi namba 15 na kufuatiliwa kwa Waziri Mkuu aliongoza kuweka udongo kwenye majeneza matatu.
Baada ya hapo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walianza kuweka udongo kwenye makaburi hayo.
Wakati majeneza yenye miili ya waliofariki ikipangwa uwanjani, Waziri Mkuu akiwa ameongozana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alielekea katika wodi walipolazwa majeruhi 15 wa ajali hiyo, na kupata maelezo kutoka kwa madaktari na majeruhi.
“Madaktari wanajitahidi, tuwe na imani tumwombe Mungu aendelee kuwalinda, tunaamini watapona, nimewajulia hali zao ni nzuri wakilinganisha na jana, tunaamini watarejea katika hali ya kawaida,” alisema.
Majeruhi wengine walikuwa wamelazwa katika wodi ya macho ambayo iligeuzwa ya majeruhi baada ya ajali hiyo.
Waziri Mkuu alitembelea kitanda kimoja baada ya kingine na kuzungumza na majeruhi ambao walisema wanaendelea vizuri na kueleza wanaridhishwa na huduma zinatolewa hospitalini humo.