Vinara ‘wapigaji dili’ Dangote hawa hapa

11Dec 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Vinara ‘wapigaji dili’ Dangote hawa hapa
  • *Magufuli awaumbua, asema atawashughulikia wanasiasa na matepeli wote walioingilia kati.

SIKU tano baada ya gazeti hili kuandika juu ya bilionea Aliko Dangote, kuja nchini kuteta na Rais John Magufuli juu ya sakata lililofanya kiwanda chake cha Saruji kilichoko Mtwara kisitishe uzalishaji,

Mfanyabiashara huyo ametua nchini na kuzugumza na kiongozi huyo wa Tanzania na kusema mradi huo hauna tatizo isipokuwa uliingiliwa na ‘wapiga dili’ ambao ameapa kuwashughulikia.

Katika video ya dakika nane na sekunde 15 iliyowekwa kwenye blogu ya Ikulu, Rais Magufuli amesema serikali haiwezi kuona ikichezewa.

“Tatazo la Watanzania ni watu wa katikati. Hapakuwa na tatizo lakini pamekuwapo watu wapiga dili kwenye mradi huu, badala ya kununua gesi moja kwa moja TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania), ambacho ni chombo cha serikali anaingia mtu katikati pale anataka naye atengeneze kamisheni.

“Tunataka eneo kwa ajili ya gati (bandari) kaeneo kadogo tu pale, watu wanataka wakalipwe Sh. bilioni 43 (bandari ya kiwanda cha Dangote Mtwara) kana kwamba watu wanachukua maeneo kule ili wakalipwe fidia.

“Kwa hiyo wapiga dili ndio walikuwa wameuingilia huu mradi na sasa hivi wameshindwa na watalegea moja kwa moja kwa sababu Dangote wamemwona mwenyewe yuko hapa na mwezi huu analeta magari 600 na yameshaanza kuja kwa ajili ya kubeba simenti na amezungumza, ninyi wenyewe mmemsikia.

“Hataagiza makaa ya mawe au ‘gypsum’ kutoka nje kwa sababu haiingii akilini kwa nchi yoyote inayotaka kujenga viwanda kutengeneza ajira, mna ‘gypsum’ na makaa ya mawe ya kutumika kwa zaidi ya miaka 200 halafu mnakwenda kununua makaa ya mawe nchi nyingine. Halafu makaa ya mawe hapa yanauzwa kwa bei ya chini kuliko makaa ya mawe yanayouzwa kutoka nje.

“Amezungumza kwamba atanunua makaa ya mawe hapa hapa na ‘gypsum’ atanunua hapa hapa. Sisi tunapeleka gypsum mpaka kwenye viwanda vya Rwanda na Congo wananunua kutoka hapa na ‘gypsum’ iko kilomita chache tu kutoka kwenye kiwanda chake halafu ukaagize nje! Amezungumza kabisa kwamba atanunua makaa ya mawe na ‘gypsum’ hapa ili watu wetu wapate ajira, watu wetu wa kusini wapate ajira na hicho ndicho tulichoahidi na amesema kiwanda baada ya mambo kadhaa kitaanza kufanya kazi kama kawaida.

“Ila wasemaji walikuwa wamejitokeza wengi wanasiasa, matapeli, na wale sisi tutashughulika nao kikamilifu kwa sababu serikali ipo, haiwezi ikachezewa na matapeli, lakini pia gesi watanunua moja kwa moja TPDC,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza kuwa: “Hawa waliokuwa wamejiingiza hapa katikati, kuna likampuni sijui linaitwa…, mimi silijui, mawaziri wanafahamu, linafutiliwa mbali ili kusudi Dangote anunue gesi ambayo ipo kwa matani kwa matani na ni kilomita mbili tu kutoka pale (kiwandani) wanunue moja kwa moja kutoka TPDC kwa bei ambayo ni ‘reasonable’ (ya kuridhisha) na yeye aende akafanye kazi.

“Mengi yaliyokuwa yanafanywa ni ya wanasiasa, wanataka kuchongea chongea mle, wanapoteza muda. Dangote mmemuona mwenyewe tena tumevaa tai zinazofanana, kwa hiyo tunamtakia kazi njema wananchi wakae mkao wa kufanya biashara tunataka kujenga Tanzania mpya, ya viwanda.

“Tumemwambia pia mbeleni aangalie namna ya kujenga viwanda vingine vya mbolea na amesema yeye yupo na anaona Tanzania ni mahali pekee pa kufanya biashara kwa sababu kisiasa tuko vizuri, tumetulia, watu wenyewe wana upendo, serikali tuko imara, inapenda watu.

Kwa hiyo yeye yuko hapa, kwa hiyo waliokuwa hawamjui Dangote ni huyu hapa (akimshika begani), tofauti yake na mimi, yeye ni tajiri mimi maskini,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Dangote alisema ameamua kuwekeza Tanzania na kwamba dola milioni 600 aliyowekeza kwenye kiwanda hicho cha saruji ni sehemu tu ya uwekezaji wake nchini.

Alisema baadhi vyombo vya habari vilikuwa vikiandika taarifa ingawa havikuingia kwa undani zaidi.

Dangote alisema kama angetaka kufunga biashara asingeagiza malori 600 ambayo awamu ya kwanza yameshafika bandarini na kwamba kabla ya kumalizika mwezi huu, yote yatakuwa yamefikishwa nchini.

“Tumeagiza malori mapya 600 na haya magari 600 ukiweka mafundi, madreva na mautingo, tunaongelea ajira nyingine 1,500. Kama tungekuwa hatuna amani na kuwekeza hapa hakuna namna ingetufanya tulete lori 600 hapa,” alisema Dangote.

“Yamekuja awamu ya kwanza na kabla ya Krismasi yote 600 yatakuwa yamewasili,… sisi hapa kazi yetu ni kutengeneza ajira, hatutaagiza kama ni makaa ya mawe au ‘gypsum’, tutatumia vilivyopo hapa, si tu kwamba tutanunua bali pia tutajaribu kushirikiana na viwanda vya hapa vinavyofanya hizo shughuli,” alisema.

Wapiga dili

Katika mahojiano maalumu na Nipashe Desemba 4, mwaka huu, kuhusu ujio wa Dangote, Mwakikishi Mkazi wa Dangote nchini, Esther Baruti, alisema kuna makundi matano yanayoupa changamoto uwekezaji wa tajiri huyo namba moja barani Afrika nchini.

Alisema kundi la kwanza ni la wapinzani wa kiuchumi hasa nchi jirani ambazo hazijafurahishwa na uwekezaji huo huku baadhi wakitenga mabilioni ya shilingi kuwashawishi watu wake wa karibu ili wamshauri ahamishie kiwanda chake kwenye nchi zao.

Kundi la pili, Baruti alisema ni la wapinzani wa kibiashara hasa kampuni zingine zinazozalisha saruji baada ya Dangote kuonekana tishio kwao kutokana na kushusha bei ya bidhaa hiyo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa kiwanda cha Dangote kimefanikiwa kushusha bei ya saruji kwa asilimia 30 tangu kilipoanza uzalishaji mwishoni mwa mwaka jana.

Kabla Dangote hajaanza kuzalisha saruji nchini, mfuko wa kilo 50 za saruji nchini ulikuwa unauzwa hadi Sh. 18,000 lakini kabla ya kusitisha uzalishaji wiki mbili zilizopita, ulikuwa unauzwa kwa Sh. 10,500.

Kundi la tatu, kwa mujibu wa Baruti, ni la wasafirishaji ambao alidai hawajafurahishwa na kitendo cha Dangote kuingiza nchini malori 30 kwa ajili ya kusafirishia saruji yake, huku akiwa na mpango wa kuingiza mengine 600.

Alisema kundi la nne ni la wanasiasa ambao wanaamini kusitisha kwa uzalishaji wa kiwanda cha Dangote cha Mtwara ni mtaji mkubwa kwao kisiasa.

"Kundi la mwisho ni la watu wa kati ambao kazi yao ni kupiga dili. Siwezi kuwataja lakini ni wengi sana.

Wananufaika na bidhaa ambazo zinatumika kuzalisha saruji. Atakuja kuwasema mwenyewe kwa Rais John Magufuli," alisema Esther siku hiyo.

Alisema pia "kuna mambo mengi tuliyokubaliana na Serikali kabla ya kuwekeza kwenye mradi huu mkubwa na hatuna tatizo na serikali. Imetupa msamaha wa kodi kwenye mambo mengi kuanzia ardhi, mafuta ya dizeli lita milioni tatu na mengine mengi.

“Kiwanda chetu cha saruji kinapigwa vita na watu wa kati (hakuwa tayari kuwataja). Mkumbuke hiki ni kiwanda kikubwa zaidi katika uzalishaji wa saruji upande huu wa Afrika Mashariki. Kuna watu wanakipiga vita kwa nia ya kuondoa uwekezaji wa Dangote hapa Tanzania.”

Baada ya taaria za kiwanda hicho kusitisha uzalishaji kuanza kuandikwa na vyombo vya habari, Mwijage, alisema serikali imebaini Dangote anapotumia dizeli, anapata hasara na akitumia gesi asilia kwa kuuziwa kwa Dola 5.14 kwa futi za ujao 1,000 ni nafuu kwa uzalishaji wa kiwanda chake.

“Sitaki kiwanda kimoja kipotee, hasara za kutoa nishati bure ni kubwa sana. Tuna viwanda vya saruji 10 kama mlezi wa wana viwanda, siwezi kumpa mmoja bure na wengine niwauzie. Namsihi anayetaka kununua gesi au makaa ya mawe akanunue,” alisema Mwijage.

Waziri huyo aliongeza: "Wawekezaji wanaendelea kuja na tumeweka kitengo cha wepesi wa kufanya shughuli, wenye matatizo au ushauri walete. Matatizo yapo kwa kuwa hakuna biashara isiyo na tatizo. Ukiona bahari haina mawimbi hilo ni dimbwi.

“Kuna viwanda 10 vya saruji nchini, hakuna upungufu wa saruji nchini… Dangote ndiyo aliyeleta mabadiliko kwenye saruji kwa bei kushuka,” alisema.

Alisema lengo la kuanzisha viwanda ni kutengeneza ajira, kupanua soko la ndani na nje pamoja na kukusanya kodi, na kwamba hayo yatafanikiwa iwapo malighafi ya nchini itanunuliwa na siyo kuagiza nje.

Uongozi wa Kiwanda cha Dangote umekuwa ukilalamika kuwa TPDC imeshindwa kukiuzia gesi kiwanda chao kwa bei ya Mtwara kwa kuwa inazalishwa eneo hilo, pia makaa ya mawe nchini hayana ubora na kunyimwa kibali cha kuagiza nje.

Mtendaji Mkuu wa Dangote Tanzania, Duggal, alisema kushindwa kupatikana kwa nishati hizo kumefanya Dangote kutumia lita 200,000 za mafuta ya dizeli kila siku licha ya ahadi ya serikali wakati wa uwekezaji kuwa kingepata nishati ya umeme kwa bei rahisi.

Kaimu Kamishana wa Madini, Mhandisi John Shija, naye alisema makaa ya mawe yaliyoko nchini yanaweza kutumika kwa miaka 200 ijayo, uzalishaji kwa sasa ni tani 60,000 kwa mwezi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Kapuulya Musomba, alisema mnunuzi mkubwa wa gesi asilia ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kwamba katika mazungumzo na Dangote alisema akitumia dizeli au mafuta mazito anapata hasara ya dola milioni tatu kwa mwezi na akitumia gesi anaokoa dola milioni tatu hadi tano kwa mwezi.

“Gesi yetu tumeweka punguzo la asilimia 25 hadi 30 kwa viwanda. Mazungumzo yetu ya mwisho alisema atanunua kwa bei ya Tanesco na ikipanda pia ataendelea kununua,” alisema.

Kina Sendeka waapishwa

Wakati huo huo taarifa iliyotolewa jana Naibu Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu, ilisema Rais Magufuli amwapisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole-Sendeka anayechukua nafasi ya Dk. Rehema Nchimbi ambaye amehamishiwa Singida.

Wengine walioapishwa na Rais Magufuli ni Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye anakuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo (Kilimo), Dk. Maria Sasabo kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Grace Martin kuwa Balozi (Mkuu wa Itifaki).

Habari Kubwa