Vinara ukiukwaji uhuru habari hadharani

03Nov 2017
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Vinara ukiukwaji uhuru habari hadharani

BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limelitaja Jeshi la Polisi, Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwa vinara wa ukiukwaji wa uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga.

Tangu mwaka 2002, baraza hilo limesema limepokea zaidi ya matukio mabaya 30 waliyotendewa waandishi wa habari ikiwamo unyanyasaji, kunyimwa taarifa, kutishwa, kubughudhiwa, kutekwa, kuuawa na kufungiwa huku kwa mwaka huu pekee yakiripotiwa matukio 20.

Kutokana na hali hiyo, MCT na washirika wake wameamua kuwapeleka mahakamani watu wanaoripotiwa kuwazuia, kuwanyanyasa na kuwapiga waandishi wa habari pindi wanapokuwa katika majukumu yao.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, aliyasema hayo jana ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Jinai dhidi ya Wanahabari.

“Mkiukaji mkubwa wa uhuru wa waandishi wa habari amekuwa serikali kupitia polisi, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, ukiachilia mbali wizara ambayo baadhi ya magazeti yaliyofungiwa yanalalamika mahakamani,” alisema Mukajanga.

Alisema MCT hairidhishwi na hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini kwa kuwa kwa kipindi cha miezi sita iliyopita magazeti matano yamefungiwa pamoja na waandishi mbalimbali wamepata misukosuko wakiwa kazini.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hofu kwa waandishi wa habari na tasnia nzima imekuwa ikiongezeka siku hadi siku hali ambayo imesababisha waandishi kutokufanya kazi zao kwa uhuru na weledi.

Mukajanga aliwataja baadhi ya waandishi wa habari waliopatwa na misukosuko wakiwa kazini  kuwa Halfani Liundi wa ITV Arusha, ambaye aliwekwa kizuizini na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara.

Wengine ni Augusta Njoji wa gazeti la Nipashe, ambaye aliandika habari za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kukamatwa kisha kuhojiwa na polisi na badaye kuachiwa kwa dhamana.

Wengine ni wapigapicha wa Kampuni ya The Guardian Ltd, Seleman Mpochi na John Badi walionyang’anywa kamera zao wakiwa kazini.

Mukajanga alisema kipindi cha miaka miwili iliyopita, kumekuwa na matumizi mabaya ya madaraka, upindishwaji wa sheria, unyanyasaji na matamshi ya vitisho kutoka kwa viongozi dhidi ya wanahabari na vyombo vyao, kunakoambatana na kufungia vyombo vya habari kwa kasi.

Habari Kubwa