Viongozi CCM mbaroni kwa tuhuma za rushwa

02Jul 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Viongozi CCM mbaroni kwa tuhuma za rushwa

VIONGOZI wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za rushwa.

Wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, Asha Makwaiya, na Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Tawi la Mshikamano, Elizabeth Itete. Mbali na viongozi hao, pia wamo wajumbe 10 wa UWT.

Mkuu wa Takukuru mkoani Shinyanga, Hussein Mussa, alisema jana kuwa viongozi na wanachama hao walikamatwa Juni 28, mwaka huu, nyumbani kwa Itete wakipokea vitu hivyo.

Alisema baada ya kupata taarifa juu ya kutokea kwa tukio hilo, maofisa wa Takukuru walifika nyumbani kwa Itete na kumkuta Makwaiya na wajumbe hao wa UWT wakiwa na vitenge, kandambili na mashuka kwa ajili ya kutoa na kupokea rushwa.

“Tulimkamata Asha Makwaiya ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, akiwa nyumbani kwa Elizabeth Itete ambaye ni Katibu wa UWT Tawi la Mshikamano, akitaka kutoa rushwa kwa wajumbe hao ili kushawishi achaguliwe au kuchaguliwa kwa aliyemtuma kuwa kiongozi katika uchaguzi mkuu,” alisema Mussa.

Aliongeza kuwa: “Tunawashikilia pia wajumbe 10 wa UWT Kata ya Ngokolo ambao tuliwakuta nyumbani kwa katibu wa UWT wakiwa na Makwaiya, wakitaka kupokea rushwa. Bado tunaendelea na uchunguzi dhidi yao kutokana na kudai kuwa waliitwa tu hawakujua kama kuna kupewa rushwa.”

Kutokana na kujitokeza kwa hali hiyo, Mussa aliwataka wananchi wa mkoa wa Shinyanga, kuendelea kutoa taarifa katika taasisi hiyo hasa katika kipindi hiki cha kuanza mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya vyama kwa ajili ya kuwania nafasi za ubunge na udiwani.

Habari Kubwa