Viongozi mbaroni tuhuma kutesa wananchi

06Jul 2020
Godfrey Mushi
Hai
Nipashe
Viongozi mbaroni tuhuma kutesa wananchi

VIONGOZI watano wa Serikali ya Kijiji cha Isuki kilichopo Kata ya Masama Kati, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wamekamatwa kwa tuhuma za kuendesha operesheni za ukatili dhidi ya wanawake ambao huwakamata na kuwacharaza viboko 60, kuwatoza fedha na kupakwa ‘washawasha’ sehemu za siri.

Kadhalika, serikali ya kijiji hicho imekiri kununua pingu ili kutekeleza amri ya wananchi kutotembea usiku, baada ya saa 2:00.

Kutokana na taarifa hizo za kukamatwa, kufungiwa na kuteswa katika mahabusu ndogo ya kijiji hicho iitwayo Golgotha, Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya, amefuta utaratibu wa sungusungu kufanya operesheni ndani ya kijiji hicho.

Pia, ameamuru kukamatwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), viongozi hao ambao ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho Rabikira Makere, mjumbe wa serikali ya kijiji, Tekla Assenga na wenyeviti watatu wa vitongoji wanaolalamikiwa kwa unyanyasaji huo dhidi ya raia.

Akieleza namna alivyokamatwa na kuteswa, mmoja wa waathirika wa ukatili huo, Neema Ng’unda, alidai baada ya kukamatwa majira ya saa 1:15 usiku, alifungwa pingu na kupelekwa katika jengo la Golgotha na kupakwa washawasha baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh. 30,000.

“Walinifuata baa (kilabu cha pombe), nikiwa nakunywa mbege nilikuwa na bibi yangu na mama yangu mdogo, wakaniambia huu sio muda wa kunywa pombe mwanamke, wakaniambia sasa hivi ni saa 2:00 wakaninyang’anya simu wakanileta hapa Golgotha.”
“Mama yangu mdogo akaambiwa anivue nguo nipakwe khafii (washawasha), nikavuliwa akanipaka washawasha.

“Wakaniambia kama hauna hela, lipa Sh. 30,000, nikamwambia sina, nikaweka simu yangu rehani, wakasema kwamba haina thamani. Mheshimiwa Mwenyekiti, akaniambia kama hauna pesa, weka saini ya kupakwa washawasha.

“Nikamwambia sawa mwenyekiti, akaandika na daftari analo na saini niliweka ya kupakwa washawasha.”

Muathirika mwingine wa ukatili huo, Ndumiswae Makere, alisema Februari, mwaka huu, akiwa kwenye baa yake, alikwenda mtu aitwaye mama Tajiri (Tekla), akiwa na mwenyekiti wa kitongoji na doria ya watu wanane, wakawaambia watu wako chini ya ulinzi akiwamo shemeji yake na kumfunga pingu.

“Tulipofika kwenye hiyo ofisi tuliwekwa pingu mimi na mtoto wa dada yangu, ikabidi nimpigie simu shemeji yangu na dada yangu wakaja wote. Wakaniambia aliyekuruhusu uuze pombe ni nani, nikasema ni uongozi wa kijiji, nikafunguliwa pingu.”

Alipoulizwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Rabikira Makere, kuhusu umiliki wa pingu na sheria kandamizi kutumika kutesa wananchi alisema: “Hili la kutotembea usiku tulipitisha hapa katika mkutano wa kijiji na wananchi waliridhia. Pingu tulinunua Moshi Mjini,” alikiri Mwenyekiti huyo.

Onesmo Munuo, akizungumza katika mkutano huo alimwomba Mkuu wa wilaya hiyo na timu yake kuwaelimisha kuhusu matumizi ya pingu.

“Mtuelimishe, hivi kweli pingu zinauzwa kama njugu? Kijiji hiki peke yake ndio kina pingu, jaribuni kutuelimisha juu ya matumizi ya pingu na unyanyasaji,” alisema Munuo.

Kwa upande wake Ole Sabaya alisema: “Hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kuwashurutisha wananchi walale saa 2:00 usiku, isipokuwa Rais John Magufuli. Ni kinyume cha utaratibu na sheria, na ni ukanyagaji wa katiba ya nchi.”

Akizungumza juzi katika mkutano huo wa dharura kusikiliza malalamiko hayo, Ole Sabaya alisema serikali imempeleka Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Jared Swai, lakini hapewi ushirikiano.

AAMURU WARUDISHE PESA

Kuhusu fedha zilizokuwa zikitozwa kutokana na ukatili huo, Ole Sabaya ameagiza Mwenyekiti wa kijiji hicho, Makere Tekla (mjumbe) na wenyeviti wa vitongoji vitatu wakamatwe na warudishe fedha zote za wananchi ambazo wamezichukua baada ya kuwatesa.

Vile vile, aliagiza kufunguliwa upya kwa kituo kidogo cha Polisi Losaa, ambacho kilifungwa ili kutoa huduma kwa wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.

“Kuanzia sasa, nisisikie sungusungu anafanya operesheni yoyote kwenye kijiji hiki, badala yake namuelekeza Ofisa Tawala, amuelekeze mshauri wa Jeshi la akiba (Mgambo).”

Habari Kubwa