Viongozi Tanesco hatihati kupoteza ajira zao

04Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Viongozi Tanesco hatihati kupoteza ajira zao

WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani, amesema mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambao hawatawaunganishia umeme kwa wateja waliolipia huduma hiyo hadi Aprili 16 mwaka huu watapoteza ajira zao.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani.

Dk. Kalemani ametoa agizo hilo mara baada ya kutembelea miradi ya umeme katika Kata ya Ntyuka jijini Dodoma ambapo amesema Desemba 30, Mwaka Jana aliagiza kuwa hadi kufikia Aprili 15, mwaka huu waliolipa gharama za kuunganishiwa umeme wawe tayari wamefikishiwa huduma hiyo.

“Tarehe 16 mwezi huu, kama kutakuwa na meneja hajawaunganishia umeme wateja waliolipia kuanzia siku hiyo ajifahamu kuwa hana kazi. Nitakuja na orodha na nitazisoma wazi kwamba huyu kuanzia leo hana kazi,” amesema Dk. Kalemani.

Aidha, amesema mameneja wanaokatakata umeme vibaya katika maeneo mbalimbali wajiandae kubeba virago ifikapo Aprili 15 mwaka huu, na katika ziara hiyo Kalemani amegundua kuwa Tanesco wanafunga transfoma moja katika maeneo yanayohitaji transfoma zaidi ya moja.

 “Maeneo ambayo umeme unakatikakatika sio Dar es Salaam sio Mbeya ziongezwe transfoma ili umeme uache kukatika, Umeme unakatika kwasababu watu wanakuwa wengi transfoma inazidiwa,” amesema Dk. Kalemani

Habari Kubwa