Viongozi wa dini Meya wakamatwa wakitoa msaada Lucky Vincent

19May 2017
John Ngunge
Nipashe
Viongozi wa dini Meya wakamatwa wakitoa msaada Lucky Vincent
  • Meya Arusha, viongozi wa dini mbaroni
  • Waandishi 10 wasombwa, waachiwa

POLISI mkoani hapa jana iliwashikilia kwa muda Meya wa Jiji la Arusha, madiwani, viongozi wa dini, waandishi wa habari na wamiliki wa shule baada ya kuwakamata katika shughuli ya kutoa rambirambi kwa Shule ya Awali na Msingi ya Lucky Vincent.

Tukio hilo lilitokea jana majira ya asubuhi wakati viongozi wa Shirikisho la wamiliki na mameneja wa shule na vyuo binafsi (Tamongsco) Kanda ya Kaskazini, walipokwenda kutoa rambirambi Shule ya Awali na Msingi ya Lucky Vincent kufuatia ajali ya gari iliyotokea Mei 6, mwaka huu na kuua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva.

Waandishi waliokumbwa na kadhia hiyo ni Zephania Ubwani (Citizen), Filbert Rweyemamu (Mwananchi), Alphonce Kusaga (Triple A Radio FM), Joseph Ngilisho (Sunrise FM Radio), Godfrey Thomas (Ayo TV), Janeth Mushi (Mtanzania), Geofrey Steven (kujitegemea), Idd Uwesu (Azam TV), Elihuruma Yohane (Tanzania Daima) na Hussen Tuta (ITV).

Akizungumza baada ya kuachiwa jana, Ubwani alisema Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, na Diwani wa Kata ya Olasiti, Alex Marti na Diwani wa Kata ya Muriet, Credo Kifukwe ni miongoni mwa vingozi wa kisiasa waliokamatwa katika tukio hilo.

Alisema anashangaa kukamatwa na polisi kwa tukio ambalo siyo kosa. Alisema wengine waliokamatwa ni viongozi wa dini na Tamongsco ambao majina yao hakuyapata mara moja, lakini wazazi hawakuwa miongoni mwa waliokamatwa.

Kwa upande wake, Rweyemamu alisema wakati wakiwa wameanza shughuli hiyo kwa sala ndani ya ukumbi wa shule hiyo, ghafla waliingia polisi na mmoja wao akawaambia wako chini ya ulinzi kwa madai kuwa mkutano huo haukuwa na kibali.

Baada ya kukamatwa waliingizwa kwenye magari ya polisi na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Mkoa kwa mahojiano. Mtangazaji wa Triple A FM Radio, Kusaga, alisema wakiwa polisi mmoja wao aliwahoji aliyewaalika kwenda kwenye shughuli hiyo.

MILIONI 18

Hata hivyo, waandishi hao waliachiwa, lakini Meya na viongozi wengine waliendelea kushikiliwa na polisi hadi wakati Nipashe ikienda mitamboni. Tamongsco Kanda ya Kaskazini, walikwenda shuleni hapo kutoa rambirambi kufuatia ajali ya gari iliyotokea Mei 6, mwaka huu na kuua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Yusuf Ilembu, jumla ya Sh. milioni 18 zilitarajiwa kutolewa na Tamongsco kwa wazazi waliofiwa. Akizungumzia tukio hilo, Ilembu alisema, polisi walifanya makosa kuwakamata waandishi wa habari kabla ya kufafanua kuwa waandishi hao walipewa lifti kwa usalama wao kutoka eneo hilo.

Wanafunzi hao walipata ajali eneo la Marera, Kata ya Rhotia, wilayani Karatu, wakienda kufanya mitihani ya ujirani mwema na wanafunzi wenzao wa darasa la saba wa Shule ya Tumaini Junior.

Wanafunzi watatu Doreen Mshana, Saada Awadhi na Wilson Tarimo ndiyo pekee waliosalimika katika ajali hiyo na sasa wanapata matibabu nchini Marekani kwa ufadhili wa Taasisi ya Samaritan’s Purse ya nchini humo.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Malera wilayani Karatu, majira ya saa tatu asubuhi wakati mvua ikinyesha, baada ya basi la wanafunzi aina ya Mitsubish Rossa lenye namba za usajili T871 BYS mali ya shule hiyo kuacha njia wakati likiwa kwenye mteremko mkali na kutumbukia kwenye korongo.

Wanafunzi hao pamoja na wengine waliokuwa katika magari mengine mawili walikuwa wakielekea Tumaini Junior kwa utaratibu ambao hufanyika kila mwaka kwa wanafunzi wa darasa la saba.

Meneja wa Shule hiyo ambayo imefungwa kwa muda, Casmir Moshi, alisema tukio hili ni baya na kubwa kutokea katika shule hiyo ya bweni na kutwa yenye wanafunzi wengi kutoka Arusha, mikoa ya jirani na Dar es Salaam, tangu ianzishwe mwaka 2006.