Viongozi wa dini watoa neno walioshindwa uchaguzi mkuu

08Nov 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Viongozi wa dini watoa neno walioshindwa uchaguzi mkuu

VIONGOZI wa dini kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wamewataka wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kukubali matokeo kwa sababu Mungu ametaka iwe hivyo.

Wakizungumza jana katika kongamano la kumshukuru Mungu baada ya uchaguzi lililobebwa na kaulimbiu ya ‘Amani yetu, Maendeleo Yetu’, viongozi hao walisema walioshindwa wakihitaji ushauri kwao, milango iko wazi.

Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe, alikumbusha kuwa katika Katiba ya nchi Ibara ya 41(7), iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais, hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.

“Maana yake ni kwamba shughuli yote imeshafungwa na wagombea wote katika kusaini maadili, yalijengwa na Katiba.

“Hakuna mamlaka nyingine ya kuchunguza kuhusu kuchanguliwa Rais, labda kwa wakati mwingine kama katiba itabadilishwa," alisema.

Askofu Kakobe alisema licha ya baadhi ya wagombea kuwataka wananchi kujitokeza barabarani baada ya uchaguzi, hakuna aliyefanya hivyo kwa sababu watu wameafiki kuwa mchakato huo umekwisha.

“Wananchi safari hii wamekuwa kama wajumbe, kimya kimya wametoa ujumbe kuwa uchaguzi umekwisha ndiyo maana wamekataa kujitokeza barabarani. Uvunjwe mguu au mkono halafu huyo aliyekuhamasisha kesho unamwona ameunga mkono juhudi," alisema.

Aliwataka wanasiasa wahitimishe vijembe na waliotangazwa kushinda wawapende waliotangazwa kushindwa kwa kuwa bila kutangazwa aliyeshindwa, wasingetangazwa kushinda.

“Ni muhimu kuzingatia tuliotangazwa kushindwa kwamba kwa mshindani yeyote ni mwiko kukata tamaa, usikate tamaa na kuona ndiyo mwisho wa mambo yote, bado yapo matumaini,” alisema.

Askofu Mkuu wa WAPO Mission International, Sylvester Gamanywa, alisema hakuna mamlaka inayokuwapo isiporuhusiwa na Mungu.

“Matokeo haya kwa pande zote yameshtua wengi na wapo ambao mioyo yao inaumia kwa sababu mbalimbali, nasaha zetu ni kuganga mioyo na kukubali matokeo kwa hiari kwa sababu ndivyo Mungu alivyotaka na kama kutahitajika ushauri, viongozi wa dini wapo,” alisema.

Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, katika mada yake iliyokuwa ikizungumzia 'Amani Msingi wa Maendeleo', alisema ili uchumi uendelee, ni lazima kusitokee uharibifu wowote katika ardhi na kuhatarisha amani.

“Kama kuna jambo lolote ama mgogoro wowote, ni vizuri tukae meza moja kuzungumza ili amani iendelee kuwapo,” alisema.

Mjumbe wa Masheikh Mkoa wa Dar es Salaam, Yusufu Diwani, aliyemwakilisha Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema kinachotakiwa ni kulinda amani.

Askofu wa Kanisa la Anglicana kutoka Zanzibar, Dk. Michael Hafidh, alisema visiwani huko wamekuwa na amani ya kutosha.

“Tunamwomba Rais asiwe na hofu wala woga tumeshamaliza uchaguzi, wengine wakiturudisha nyuma ni wao, sisi tunakwenda mbele, uchaguzi ulikuwa wa amani, tunamwomba Rais, baraza atakalolichagua, alichague kwa kufanya kazi, kazi yetu ni kumwombea,” alisema.

Askofu Charles Salala wa AICT Dayosisi ya Pwani, katika mada yake ya kupokea matokeo kwa amani, alisema neno hekima limebeba maana ya uwezo wa akili aliyonayo mtu kuongoza na kutoa uamuzi ulio sahihi.

Alisema kila nchi ina matatizo yake na watu wake ndiyo wanaotakiwa kuyamaliza, hivyo sera ya kuyamaliza kwa kutumia taifa lingine haoni kama ni sawa.

Katibu wa Jumuiya ya Isimailia, Mahabubu Kasimu, alisema duniani kuna watu wanaiangalia Tanzania kwa furaha, wivu na wengine kuchokonoa na kuleta uchochezi.

“Watanzania tuache ushabiki, vijembe mitandaoni, tushikamane na viongozi wetu ili maendeleo yaje kwa kasi kama tunavyoyahitaji,” alisema.

Habari Kubwa