Viongozi wahimizwa kuwa chachu mapambano VVU

11Jan 2019
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
Viongozi wahimizwa kuwa chachu mapambano VVU

VIONGOZI wa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) (KONGA), waratibu wa Ukimwi na watendaji wa baraza wamehimizwa kuwa chachu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kuhakikisha wanawafikia walengwa ili kuinufaisha jamii.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Thomas Rutachunzibwa, alitoa rai hiyo wakati wa kikao cha kuandaa mpango kazi na bajeti ya mradi wa Sauti Yetu, Kanda ya Ziwa iliyozijumuisha wilaya za Nyamagana, Ilemela, Musoma, Kahama, Sengerema, Nzega, Igunga na Muleba.

Alisema mradi wa Sauti Yetu ni muhimu kwa ajili ya kuzuia maambukizi mapya ya VVU na kuchangia katika uboreshaji wa utolewaji wa huduma za Ukimwi katika ngazi ya afya na jamii kwa kuhamasisha upimaji na uzingatiaji matumizi sahihi ya dawa pamoja na upimaji wa wingi wa virusi mwilini na kuhamasisha wenza kupima.

"Wito wangu kwenu ni kuwa mradi huu uwe chachu ya mapambano dhidi ya Ukimwi katika halmashauri zetu, naamini endapo tutatumia ruzuku hizo vyema mradi huu basi hapatakuwa tena na maambukizo mapya katika jamii zetu, tutaongeza idadi ya watu waliopima na kutambua hali zao za maambukizi ya VVU," alisema Rutachunzibwa.

Naye Mwenyekiti wa baraza la watu wanaoishi na VVU (NACOPHA), Leticia Mourice, alisema NACOPHA kupitia ufadhili wa watu wa Marekani imefanikiwa kutoa ruzuku ya Sh. 103,463,310 kwa konga nane zinazofikiwa na mradi katika mwaka wa 2017/2018.

Alisema fedha hizo zimekuwa zikitumika na konga kufanya shughuli za uhamasishaji wa upimaji wa virusi vya Ukimwi na kuzingatia vyema huduma za Ukimwi na kuhamasisha watoro wa dawa kurudi kwenye tiba, kulipa nauli za mawakili tiba, timu za waratibu wanaoshughulikia mradi ngazi ya wilaya chini ya usimamizi wa halmashauri.

"Changamoto kubwa ni pale mtu anabadilisha anwani yake na kudanganya, jambo hilo linatupa ugumu wa kumfuatilia kwa ukaribu, lakini kama mtu akiwa na amani ya moyo na hofu ya mwenyezi Mungu kila kitu kitakwenda vyema," alisema Mourice.

Ofisa Mtendaji Mkuu NACOPHA, Deogratius Rutatwe, alisema lengo kubwa ni kufanikisha juhudi za serikali kufikia malengo ya kitaifa ya 90-90-90 ili kuwezesha watu wanaoishi na virusi kushiriki katika ngazi tofauti za maamuzi na utekelezaji wa sera mbalimbali.

Aliongeza kuwa japo kuwa bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo baraza kutambulika kwenye ofisi za waganga wakuu ili kuleta umoja utakaoleta tija na mafanikio.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Mwenyekiti wa Konga ya Musoma, Abdallah Masondole, alisema watatenda kazi zao vizuri na kuwafikia walengwa wote pamoja na kuhakikisha wanatimiza lengo hivyo jamii itambue umuhimu wa kupima na kutambua afya zao na kushiriki kutoa elimu kwa sababu upimaji ni bure na wa hiari.