Viongozi watakiwa kufanya tafiti kutatua changamoto

18Jan 2022
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe
Viongozi watakiwa kufanya tafiti kutatua changamoto

MKUU wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Nchini (NDC), Meja Jenerali Ibrahim Mhona, amesema viongozi wana wajibu wa kutoa majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi wanaowaongoza kwa kufanya tafiti mbali mbali za kutosha kwa ajili ya kulisaidia taifa.

Mhona ametoa kauli hiyo, mkoani Mtwara wakati akiwaongoza wanafunzi wa kozi ya 12 ya mwaka 2021/22 ya Chuo Cha NDC katika kozi ya Mafunzo kwa vitendo kuhusu masuala ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, kilimo na viwanda walio katika ziara ya siku saba mkoani humo kwa ajili ya kuoanisha mafunzo wanayopata darasani na uhalisia wake katika ngazi za utekelezaji

Ziara hiyo iliyohusisha wanafunzi kutoka katika nchi za Zambia, Burundi, Kenya, Uganda na Tanzania, Mhona amesema Utafiti siku zote unatoa matokeo chanya juu ya njia ya kutatua changamoto zilizobainika.

Akiwa katika kituo cha utafiti cha mazao ya kilimo TARI Naliendele, amesema ni imani yake utafiti unaofanywa kwa ajili ya zao la korosho umelenga kuleta matokeo makubwa yatakayowasaidia wakulima kuwa na tija katika kilimo chao.

“Kwa hiyo ni imani yangu utafiti huu utaleta matokea makubwa katika zao la korosho na utawafanya wakulima walime mazao bora na itakuwa ni bora nimefurahi zaidi kuona sasa wanafanya mpaka utafiti wa muunganiko wa mazao na ninahakika mpaka tunamaliza siku zetu tutakuwa tumeelimika,”amesema Mhona.

Amesema katika mkoa wa Mtwara changamoto waliyoibaini ni katika suala zima la elimu na kueleza kuwa mkoa huo haufanyi vizuri kwa kuchangiwa na uhalisia wake.

Ameongeza elimu imekuwa inaachwa kwa viongozi peke, huku jamii ikijiweka kando

“Unapozungumzia suala la elimu inapaswa kukabiliwa kwa pamoja kwa maana ya wazazi wawajibike , walimu wawajibike, wanafunzi wawajibike na viongozi kwa nafasi yao watekeleze wajibu wao lakini tukiliacha jambo hili kwa viongozi pekee si sawa,” amesema.

Ameongeza kuwa ni wakati wa kuchangamsha akili kwa ajili ya kujua ni namna gani mkoa utafanikiwa kuwa na hamasa ya juu katika suala zima la elimu.

Kanal Joseph Mtakige kutoka Kenya, ambaye ni mmoja wa wanafunzi walio katika ziara hiyo ya kujifunza, amesema Utafiti unaofanywa katika kituo cha Tari Naliendele, utasaidia nchi mbalimbali.

"Tanzania ikiwa na chakula cha kutosha Kenya itafaidika Uganda Itafaidika na hata wengine watafaidika kwa hiyo utafiti ni muhimu na sisi sote tuungane pamoja kusaidia nchi zetu kwani mwelekeo tunaohitaji ni kuongeza uchumi wan chi zetu kwa kuwa na eneo dogo la kilimo linalotoa matokeo makubwa,” amesema.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia jenerali Marco Gaguti, akizungumza mbelea ya ugeni huo, amesema mkoa wa Mtwara umejipambanua kuwa kituo cha maendeleo ya kusini mwa Tanzania na kuwa ziara hiyo ya mafunzo itawapa fursa wahusika kutathmini na kushauri pale ambapo wataona panahitaji kuwekwa mkazo zaidi.

Habari Kubwa