Vipaumbele bajeti 2021/22

11Jun 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Vipaumbele bajeti 2021/22

SERIKALI imeanika vipaumbele katika bajeti yake ya mwaka 2021/22, huku ikisema vinalenga kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Akiwasilisha bungeni jana bajeti kuu ya serikali kwa mwaka huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema bajeti itajielekeza katika utekelezaji wa vipaumbele hivyo kwenye maeneo matano ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22.

Alitaja maeneo hayo ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

Alisema ili kuwa na uchumi shindani na shirikishi, serikali itajielekeza katika kugharamia miradi ambayo itajikita katika kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa, kusimamia utulivu wa viashiria vya uchumi jumla, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Pia kuchochea uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje na kuendeleza miundombinu na huduma za reli, barabara za kufungua fursa za kiuchumi, kuunganisha nchi jirani, kupunguza msongamano mijini na barabara za vijijini, madaraja, usafiri wa majini na angani, mageuzi ya TEHAMA pamoja na kutekeleza mradi wa Tanzania ya Kidijitali, nishati, bandari na viwanja vya ndege.

Alisema eneo hilo limetengewa Sh. trilioni 7.44 ikijumuisha Sh. trilioni 3.13 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kielelezo.

Pia alisema katika eneo la kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, msukumo utawekwa kwenye miradi ya viwanda inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Alisema bajeti hiyo itajielekeza katika kugharamia miradi na programu inayolenga kuboresha huduma za utalii, fedha na bima pamoja na kuendeleza viwanda vya uzalishaji wa dawa muhimu na vifaa tiba ambapo Sh. trilioni 1.38 zimetengwa kugharamia utekelezaji wake.

Alisema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ikiwamo kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Biashara na Uwekezaji (Blueprint) ambapo eneo hilo limetengewa Sh. bilioni 31.6.

"Serikali itaendelea kupanga, kupima na kumilikisha ardhi mijini na vijijini, kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji na kuendelea na utekelezaji wa programu za kulinda mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi, Sh. trilioni 4.43 zimetengwa," alisema.

Waziri huyo alisema jumla ya Sh. bilioni 50.5 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia programu inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasilimali watu katika ngazi zote za elimu.

Alisema serikali itatekeleza miradi mingine ya uboreshaji wa miundombinu ambayo itagharamiwa na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Alitaja miradi hiyo ni Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) wa kukabiliana na mafuriko kwenye Bonde la Mto Msimbazi utakaogharimu dola za Marekani milioni 120.

Pia alisema mradi wa pili unahusisha uboreshaji wa barabara za kukuza fursa shirikishi za kijamii na kiuchumi ambapo Benki ya Dunia itatoa dola za Marekani milioni 300 na mchango wa serikali ni dola za Marekani milioni 50 na unalenga unalenga kuboresha barabara za vijijini katika maeneo yenye tija kubwa ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.

MAJIJI NA MIJI

Alisema serikali imeanza mazungumzo na Benki ya Dunia kupitia dirisha la International Development Association (IDA) kwa ajili ya mradi wa uboreshaji miundombinu katika majiji na miji 45 ambapo utekelezaji wa mradi huo utaanza katika mzunguko wa 20 (IDA 20) unaotegemewa kuanza Julai 2022 na utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 500 na utahusisha ujenzi wa miundombinu ya msingi ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi wa miji husika.

Habari Kubwa