Viroba vya mil. 130/- vyakamatwa

11Mar 2017
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Viroba vya mil. 130/- vyakamatwa

MSAKO wa kukamata pombe kali aina za viroba mkoani Dodoma umeshika kasi, baada ya Jeshi la Polisi kukamata shehena yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 134.9.

Polisi walikamata shehena hiyo ya viroba kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) na Mamlaka ya Mapato Tanzani (TRA).

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lazaro Mambosasa, alisema walikamata katoni 2,199 katika wilaya za Dodoma na Mpwapwa zenye thamani ya Sh. 134,954,500.

“Huo ni mwendelezo wa oparesheni ya kutekeleza agizo la Serikali la kukamata wauzaji, wasambazaji, na watumiaji wa pombe iliopo katika vifungashio vya plastiki maarufu kwa jina la viroba ambayo imepigwa marufuku tokea Machi Mosi mwaka huu,” alisema Mambosasa.

Aliwataja waliokamatwa na bidhaa hiyo kuwa ni mkazi wa Area C, Consolata Mallya (58) kutoka kampuni ya Cowike Enterprises LTD, ambaye alikutwa na viroba Original na katoni 421, na Zed 1248.

Wengine ni mkazi wa Mpwapwa, Jobu Timoth, ambaye alikutwa na viroba katoni 62.5 na Siloya Mbonyi, wa kampuni ya Takawedo ambaye alikutwa na katoni 444.

Aliwataka wafanya biashara wa dawa za kulevya kuacha mara moja biashara hiyo kwa sababu sio halali.

“Tunawaomba wafanyabiashara waache biashara hiyo haramu, Jeshi la Polisi halitakuwa na huruma kwa mfanyabiashara yeyote atakayekutwa na bidhaa hiyo,” alisema Mambosasa.

Aidha aliagiza wafanya biashara hao, kuacha kutoa shehena hizo ambazo wamekutwa nazo hadi pale watakapopewa maelekezo toka Jeshi la Polisi.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Consolata Mallya, alisema: “Naheshimu agizo la Serikali, siwezi kuviuza nitasubiri maelekezo kutoka Jeshi la Polisi.”

Habari Kubwa