Vitambulisho machinga sokoni Dar mkanganyiko

12Jun 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Vitambulisho machinga sokoni Dar mkanganyiko

UGAWAJI wa vitambulisho kwa wajasiriamali (machinga)  jijini Dar es Salaam kwenye masoko, umejaa hofu nyingi, ikiwamo viongozi waliokuwa wavigawanye kuvisusia, masoko yakivihofia kuwa vitawaondolea tozo na kuyakosesha mapato.

Wafanyabiashara wadogo wakiwa katika shughuli zao katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam jana, bila ya kuwa na vitambulisho vya biashara vilivyotolewa na Rais John Magufuli. PICHA: JOHN BADI

Lakini si hivyo, kuna baadhi ya viongozi wanaodai vinawahusu wanaozunguka na bidhaa na si walioko sokoni na kuibua maswali kadhaa, kama kipi ni kipi?

Desemba mwaka jana, serikali iliagiza vitambulisho hivyo vitolewe kwa wafanyabiashara na wamachinga wenye mitaji iliyo chini ya Sh. 4,000,000.

Utafiti uliofanywa na Nipashe hivi karibuni katika masoko mbalimbali yakiwamo ya vyakula ulibaini mambo kadhaa kwa mfano, baadhi ya viongozi wanaohusika wanadai kuwa hawavigawi kwa sababu hawahusiki kwani kuna asasi yenye jukumu hilo.

Aidha, viongozi masokoni wanahisi pia kuwa kuanza kuvitoa, vitasababisha kukosa fedha za kugharamia huduma masokoni. Aidha, manispaa zinalaumiwa kuwa hazijalizungumzia suala hilo na kulitolea ufafanuzi.

Khalifan Mandamo, Mwenyekiti wa Soko la Chakula  Mwenge, aliliambia gazeti hili kuwa anahofia kuchukua vitambulisho hivyo kwa sababu masoko yameunganishwa na Muungano wa Masoko Mkoa wa Dar es Salaam (Mumada), ambao ndiyo msimamizi.

“Baada ya serikali kutangaza kuhusu vitambulisho hivyo, tuliitwa serikali za mitaa kuzungumzia suala hili, lakini tuliwaeleza kuwa hatujajua kama tutavichukua kwa sababu wasemaji wakuu ni Mumada, wakisema tuchukue tutafanya hivyo,” alisema Mandamo.

MKANGANYIKO

Mandamo alieleza kuwa alipofuatilia alibaini kuwa kuna mambo yamejificha kwenye utoaji wa vitambulisho hivyo kwani baadhi ya viongozi wanahisi kuwa vikitolewa wafanyabiashara hawatalipa ushuru, hivyo kutishia kukosa mapato masokoni na halmashauri.

Alisema kila siku wafanyabiashara hutozwa Sh. 200 ambazo Sh. 100 hubaki sokoni na nyingine inaingia kwenye mfuko wa Manispaa.

“Tukisema tuvichukue hofu yetu ni hii manispaa itatutambua? Itachukua takataka na kusafisha soko maana huleta gari kwa sababu tunalipa ushuru. Suala hili la vitambulisho tumeshalifikisha Mumada, lakini hadi sasa hawajatupa mrejesho,” alisema Mandamo.

MANISPAA LAWAMANI

Mwenyekiti wa Muungano wa Masoko Mkoa wa Dar es Salaam (Mumada), Mohamed Mwekya, akizungumzia suala hilo, alisema kinachoendelea kwenye vitambulisho vya wamachinga ni kukosekana ufafanuzi sahihi.

Alisema viongozi  wa manispaa hawajawafafanulia viongozi wa masokoni kuhusu utekelezaji wa agizo la serikali la vitambulisho.

“Mumada tunapenda wanachama wetu wote wapate vitambulisho ili waondokane na ushuru wanaotozwa kila siku. Huu ni gharama ikilinganishwa na vitambulisho vya serikali ambavyo wanalipa Sh. 20,000 kwa mwaka mzima,” alisema Mwekye.

Aidha, kwa mujibu wa maelezo yake, baadhi ya viongozi wa masoko waliowasiliana naye, aliwaelekeza wachukue vitambulisho, hivyo lakini walio wengi hawajavichukua.

“Viongozi wa masoko ya Kisiwani, Mwananyamala, Magomeni na Kawe  wote walinipigia simu nikawaambia Mumada inabariki suala hilo la vitambulisho. Hata masoko mengine yafanye hivyo sisi hatuna kizuizi kwenye suala linaloleta unafuu kwetu,” alisisitiza.

Mwekya aliwashutuma baadhi ya viongozi wa manispaa na watendaji wa serikali za mitaa kuwa ndiyo wanaochelewa kutoa ufafanuzi unaoeleweka kuhusu vitambulisho hivyo na kuwakosesha watu wa masokoni kuvipata.

“Wito wangu kwa  viongozi  na wafanyabiashara masokoni, chukueni vitambulisho hii ni fursa ambayo imetolewa na mkuu wa nchi Rais John Magufuli na  itatoa unafuu kwa sababu wapo wanaouza mchicha, lakini gharama ya kulipa ushuru ni kubwa kuliko wanachokiingiza,” alisema Mwekye.

UKWELI UKO WAPI?

Meneja wa soko la ndizi Mabibo-Urafiki, James Msulya, akiwa sokoni hapo aliiambia Nipashe kwenye mahojiano kuwa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, aliwatembelea na kuwaambia vitambulisho hivyo haviwahusu walio sokoni.

“Wale ambao hawapo ndani ya masoko, wanaofanya shughuli zao barabarani na maeneo yasiyo rasmi ndiyo wanaohusika na vitambulisho hivyo na siyo sisi,” alisema.

“Ofisi yetu tulikuwa na vitambulisho zaidi ya 5,000, lakini baada ya tafsiri hii ya Polepole kuwa hatuhusiki, tumewagawia wengine,” alisema Msulya.

 Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, walisema kuwa, baada ya kufuatilia suala hilo kwenye uongozi waliambiwa soko la Mabibo halihusiki na vitambulisho hivyo.

“Tumeuliza viongozi wamesema sisi wa masokoni tunaendelea na utaratibu wa utozaji wa ushuru. Tunatamani na sisi tulipe Sh. 20,000 tupate vitambulisho ili tuachane na tozo hizi ambazo kwa mwaka ni zaidi ya Sh.100,000 tunazolipia,” alisema mmoja wao.

Mmoja wa wauza matunda sokoni hapo, alisema hofu iliyopo masokoni ni kwamba watakapowapa vitambulisho hivyo manispaa zitakosa mapato yao.

Mwenyekiti wa Soko la Shekilango, David Mrisho, kwa upande wake alisema alifuatilia vitambulisho kwa  Ofisa Mtendaji Kata ya Ubungo, Isiaka Waziri, aliyemweleza kuwa haviwahusu wafanyabiashara wa masokoni,” alisema.

Mrisho alisema mtendaji alimwambia hawahusiki na vitambulisho hivyo kwa sababu kuna utaratibu wa kulipa tozo ambazo kwa siku ni Sh. 200, kwa mwezi Sh. 6,000 na kwa mwaka 72,000.

“Kama kiongozi sikuamini. Nilichokiona hapa ni kwamba Rais Magufuli alivyoingilia suala la vitambulisho, kuna baadhi ya halmashauri zinaona kama vile wameporwa mapato, mfano mimi ni fundi cherehani ninatakiwa kuwa na leseni kwa hiyo nikipewa kitambulisho, hizo tozo sitatoa,” alisema Mrisho.

Alisema sokoni Shekilango kuna wafanyabiashara wadogo wasiopungua 500, wakiwamo washonaji, wauza kuku, mboga mboga na wachinjaji.

Aidha, pamoja na majibu hayo ya mtendaji huyo, wameona katika Wilaya ya Arumeru, Mkuu wa Wilaya hiyo, Jerry Muro, akipita masokoni kuuza vitambulisho.

“Nimesikia hata Wilaya ya Kinondoni, wenzetu Magomeni wanavitoa, iweje kwa Wilaya ya Ubungo?

Juliana Kitenge, anayeuza mboga aliomba utoaji wa vitambulisho uwafikie  sokoni hapo kwa sababu biashara wanazofanya zipo chini ya mtaji wa milioni nne.

VIONGOZI WANENA

Wakati wafanyabiashara wakitoa madai yao, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, aliliambia gazeti hili kuwa wilaya yake imeshagawa vitambulisho 35,000 kwa wamachinga wakiwamo wa masokoni na bado uhitaji upo.

“Wilaya ya Kinondoni kupitia watendaji wangu tumeshagawa vitambulisho 35,000 wakiwamo wafanyabiashara masokoni. Vimefika Tegeta Nyuki tumetoa zaidi ya vitambulisho 400, Mwenge wamepewa zaidi ya vitambulisho 3,000 na maeneo mengine ya wamachinga,” alisema.

Kadhalika, Chongolo alisema licha ya kugawa vitambulisho hivyo  kuna uhitaji na kila anayefika ofisini anavitaka, hivyo wamekuwa na utaratibu wa kuazima kwa wenzao ambao bado wanavyo.

Ofisa Masoko Manispaa ya Ilala, Frank Kibika, alisema baadhi ya watu masokoni hawajachukua vitambulisho hivyo na kwamba wanaendelea kutozwa ushuru wa Sh. 200.

 “Kuna ambao wamechukua na wengine labda kwa kuona mitaji yao ni juu ya Sh. 4,000,000  hawajachukua, hawa tunawatoza ushuru kama kawaida kwa ajili ya kuendesha masoko.

Utaratibu wa vitambulisho ni kwamba mtu akiwa nacho anatakiwa akivae ili atambulike, wale wasiokuwa navyo tunawatoza,” alisema Kibiki.

Alitaja changamoto ya  baadhi ya watu wenye maduka kuchukua vitambulisho wakati mitaji yao ni juu ya milioni nne, hivyo wamepawa elimu ili wakate leseni.

 Agizo la kutoa vitambulisho lililotolewa na Rais mwaka jana katika mkutano na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kujadili namna ya kuboresha mazingira ya ukusanyaji mapato. Aidha, aligawa vitambulisho 670,000 kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.

Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa mfanyabiashara yeyote ambaye mapato yake kwa mwaka hayazidi Sh. 4,000,000 atakayekuwa na kitambulisho hicho asibughudhiwe.

Baada ya maagizo hayo kila mkoa ulikabidhiwa vitambulisho ili kutekeleza agizo hilo.

Habari Kubwa